Bunge la Seneti la nchini Kenya limepitisha kura ya kumuondoa madarakani aliyekuwa Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua.
Mwanasiasa huyo, alikuwa anakabiliwa na mashitaka 11, na iliwahitaji maseneta hao 67, kupitisha walau shitaka moja tu; ili Gachagua ang'oke madarakani.
Oktoba 17, jumla ya Maseneta 49 walipiga kura ya kumuondoa madarakani aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua kwa ukiukwaji mkubwa wa katiba ya nchi hiyo.
Mwanasiasa huyo alikuwa akikabiliwa na mashitaka 11, huku akishindwa kutokea na kujitetea mbele ya Bunge la Seneti Oktoba 17, baada ya wakili wake kusema kuwa yuko hospitali akipokea matibabu.
Kulingana na katiba ya Kenya, Naibu Rais anafikia ukomo wa nafasi hiyo baada ya kuondolewa na Bunge la Taifa na Bunge la Seneti la nchi hiyo.
Makosa matano, likiwemo la ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Kenya yalitosha kabisa kumuondoa madarakani Gachagua, ambaye amehudumu nafasi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini humo, tangu Septemba 2022.
Makosa mengine yaliyomuondoa Gachagua madarakani ni pamoja na kukiuka Ibara ya 160 (1) ya Katiba ya nchi hiyo, kwa kudharau maamuzi ya mahakama.
Kulingana na tangazo la Serikali lililochapishwa na Spika wa Seneti, Amason Jeffah Kingi mara baada ya kuondolewa madarakani, Gachagua pia anatuhumiwa kupandikiza chuki za kikabila, ambacho ni kinyume na sheria za nchi hiyo.
Gachagua, pia amehukumiwa kwa makosa ya kuwadharau na kuwadhihaki wafanyakazi wa Idara ya Intelijensia ya Kenya.
Naibu Rais huyo wa zamani, pia alikabiliwa na shitaka la kujilimbikizia mali, zenye thamani ya dola milioni 40.3 ndani ya miaka miwili, tangu alipoteuliwa kuhudumu nafasi hiyo.
Gachagua alichaguliwa kama mgombea mwenza wa Rais William Ruto katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 na aliapishwa Septemba 13, 2022.