Bunge la Seneti nchini kenya limeamua kusikiliza hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua katika kikao cha mashauriano kitakachofanyika Oktoba 16 na 17, 2024.
Bunge limechagua hili baada ya wazo la Tume la kusikiliza hoja hii kukataliwa.
"Ninawaomba wajumbe kukubaliana nami kwamba tuchague maseneta 11 kati ya maseneta wetu wenye hekima na wanaoaminika kutoka pande zote mbili za Bunge kuzingatia hoja hii," Aaron Cheruiyot kiongozi wa upande wa masenata wengi bungeni alikiambia kikao cha bunge la seneti.
Hoja imepingwa
"Hili ni jambo ambalo ni la kipekee na limeibua hisia za watu wengi na kwa hivyo Mheshimiwa Spika kutokana na hisia kali hasa kwa upande wa wachache bungeni nakataa kwa heshima kuundwa kwa tume hiyo," Naibu Kiongozi wa upande wa maseneta wachache bungeni Edwin Sifuna alipinga.
Gachagua anashutumiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa katiba, kumdhoofisha Rais, kuhujumu ugatuzi, kujipatia mali kinyume na utaratibu, kumshambulia jaji hadharani, kumtisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ugavi wa Dawa nchini (KEMSA), kuendeleza ukabila na kutomtii Rais, miongoni mwa mashtaka mengine.
Muswada huo umekuja katika Bunge la Seneti baada ya Bunge la Taifa kupiga kura ya kumuondoa katika madaraka Gachagua Oktoba 8, 2024.
Wabunge 281 walipiga kura kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua huku 44 wakikataa asiondolewe.
Seneti inaweza kumuokoa Gachagua iwapo atafanikiwa kuwainua maseneta 23 ili kushinda hoja iliyofadhiliwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Bunge la Seneti lina wanachama 47 kila mmoja aliyechaguliwa na wapiga kura waliojiandikisha wa kaunti, kila kaunti ikiunda eneo bunge la mwanachama mmoja.
Seneti itajadili hoja hiyo, na kisha itaamua ikiwa kuna sababu za kutosha za kumuondoa Naibu Rais.