Bunge la Kenya lapiga kura ya kumuondoa Rigathi Gachagua madarakani

Bunge la Kenya lapiga kura ya kumuondoa Rigathi Gachagua madarakani

Wabunge 281 wameunga mkono hoja ya kumtoa Naibu wa Raisi wa Kenya, Rigathi Gachagua mamlakani.
#NDY90 : Parliament debates impeachment motion against deputy president / Photo: AFP

Na Mustafa Abdulkadir

Bunge la Taifa nchini Kenya limepiga kura ya kumng’atua Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua madarakani.

Wabunge 281 wamepiga kura ya ndio kuunga mkono hoja ya kuondolewa mamlakani, huku wengine 44 wakipinga kutolewa kwake.

Gachagua amewasili bungeni jioni ya leo ili kujitetea kwa tuhuma 11 zinazomkabili.

Amepewa nafasi ya kujitetea kwa muda wa saa mbili, hata hivyo wabunge wa nchi hiyo hawakuonekana kuridhishwa na hoja zake za kujitetea.

Gachagua ana nafasi nyingine ya kujitetea mbele ya bunge la seneti na baadaye kujua hatma yake ya mwisho.

'Upataji wa mali haramu'

Bunge la Seneti lenye wabunge 67 pia litasikiliza mashtaka hayo, na ikiwa zaidi ya theluthi mbili - au wabunge 45 - watapiga kura kumshtaki Gachagua, naibu rais atalazimika kuondoka ofisi yake.

Miongoni mwa sababu nyingine, Gachagua anatuhumiwa kujipatia utajiri wa thamani ya shilingi bilioni 5.2 za Kenya, au dola milioni 40.3 za Marekani, kinyume cha sheria katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mwengi Mutuse, mwasilishaji wa hoja ya kumtimua Gachagua, anasema katika miaka miwili iliyopita, naibu wa rais alipokea mshahara wa shilingi milioni 24, au dola 186,000 za Marekani.

Mutuse aliongeza kuwa katika maandalizi ya uchaguzi wa urais wa Agosti 2022, Gachagua alitangaza utajiri wake kuwa shilingi milioni 800, au dola milioni 6.8 za Marekani.

TRT Afrika