Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, imefungua mazungumzo na nchi jirani ya Uganda kuhusu uwezekano wa kutumia bomba la mafuta ghafi nchini humo kusafirisha mafuta ya petroli, Waziri wa Hidrokaboni amesema.
Bomba kubwa la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (Eacop) linakwenda umbali wa maili 898 kutoka magharibi mwa Uganda, ambako ni jirani na DRC, hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania. Kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa ya Total Energies na kampuni ya nishati ya Uchina ya CNOOC International wana hisa katika mradi wa $5bn.
Bomba hilo limezua mzozo juu ya wasiwasi wa mazingira na hali ya hewa lakini Uganda na Tanzania wanasema wanalihitaji kwa maendeleo ya kiuchumi. Uganda inatarajia kuanza uzalishaji baada ya miaka miwili.
Katika taarifa yake, Wizara ya Hydrokaboni ya DRC ilisema waziri Didier Budimbu alikutana na mwenzake wa Uganda kwa mazungumzo kuhusu upatikanaji wa bomba hilo.
Nchi hizo mbili zinashiriki bonde la Albertine Graben ambapo vitalu vya gesi ya mafuta vimepatikana. DRC inatumai mafuta yake ghafi yanaweza kusafirishwa kupitia bomba hilo.
"Uganda ilikubali hitaji muhimu la DRC kufikia Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa ajili ya usafirishaji wa mafuta ghafi yatakayozalishwa kutoka kwenye vitalu vya utafiti wa mafuta vilivyoko Albertine Graben katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," taarifa hiyo ilisema.
Taarifa hiyo ilisema timu za kiufundi za pande zote mbili zitajadili na kuandaa ripoti zitakazowasilishwa kwa mawaziri hao wawili ambao watatoa taarifa kwa marais wa nchi hizo kuhusu kusaini Mkataba wa Makubaliano.