Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine atafanyiwa upasuaji, wakili wake alisema Jumatano, siku moja baada ya kupata jeraha mguuni wakati wa tukio ambalo chama chake kiliripoti kuwa alipigwa risasi na ikabainika kuwa lilikuwa ni bomu la machozi.
Kiongozi huyo wa upinzani alikuwa katika mji wa Bulindo, karibu kilomita 20 (maili 12) kaskazini mwa mji mkuu Kampala, ambapo chama chake cha National Unity Platform (NUP) kilisema tukio hilo ndipo lilipotokea.
Lakini siku ya Jumatano wakili wake, George Musisi, aliiambia AFP kwamba Wine "Yuko hatarini, lakini kulingana na madaktari, atafanyiwa upasuaji ili kuondoa vipande vinavyoshukiwa kuwa kwenye mtungi wa gesi ya machozi, vilivyompiga."
Katika hali ya kutatanisha baada ya tukio la Jumanne, kiongozi huyo wa upinzani, jina lake halisi Robert Kyagulanyi, alikimbizwa katika hospitali ya Nsambya jijini Kampala, huku picha na video zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 42 akilia kwa maumivu.
'Shambulio la mabomu ya machozi'
Musisi anadai kisa hicho kilitokea wakati polisi "bila kubagua" walipofyatua mabomu ya machozi kwa kikundi kidogo cha wafuasi katika mji wa Bulindo, ambapo Wine alikuwa katika mkutano.
“Bomu la machozi lilimlenga na kulipuka na kumjeruhi mguuni,” alisema.
Musisi alilaani kisa hicho na kusema polisi wamewakamata wafuasi wanne wa chama hicho wakati wa ghasia hizo.
Polisi wa Uganda walisema Jumanne kwamba wataanzisha uchunguzi kuhusu "tuhuma za kupigwa risasi na matukio yoyote yanayohusiana nayo."
Taarifa hiyo, iliyochapishwa kwenye X, ilisema maafisa katika eneo la tukio walikana toleo la wapinzani, wakisema Wine alijikwaa na kujijeruhi wakati akiingia kwenye gari lake.