Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa watakutana kwa mashauriano ya faragha ili kujadili hali mgogoro kati ya Ethiopia na Somalia chini ya kipengele cha ajenda ya "Amani na Usalama Afrika."
Ufaransa ambayo ndiyo rais wa baraza, imepanga mashauriano baada ya Somalia kuomba mkutano wa dharura katika barua ya Januari 23 kwa Baraza hilo.
Katika barua hiyo, Somalia imetaja Kifungu namba 35 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambacho kinasema kuwa nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa “inaweza kuwasilisha mzozo wowote, au hali yoyote...(yaani, ambayo inaweza kusababisha msuguano wa kimataifa au kuzua mzozo) mbele ya Baraza la Usalama au Baraza Kuu.”
Ombi la Somalia katika mkutano wa Baraza la Usalama linakuja huku nchi hizo zikikataa mkataba ambao ulitiwa saini kati ya nchi jirani yake ya Ethiopia na eneo la Somaliland.
Mkataba huo unakubali Ethiopia kukodisha sehemu ya ukanda wa ufuo wa bahari katika Bahari Nyekundu kutoka Somaliland, lakini Somalia imekataa ikidai kuwa Somaliland ni sehemu ya Somalia na Ethiopia haifai kuingia mikataba nayo.
Somaliland ni eneo la kaskazini mwa Somalia ambalo limejitambulisha kuwa huru lakini halitambuliwi na Umoja wa Afrika wala Umoja wa Mataifa.
Katika barua yake ya Januari 23 kwa Baraza la Umoja wa Mataifa, Somalia imesema kuwa makubaliano hayo, "yanafanya ukiukwaji usio halali" wa mamlaka na uadilifu wa eneo la Somalia, ambalo Somaliland "ni sehemu yake."
Ethiopia kwa upande wake imesema iko na haki ya kupanga ufuo wa bahari kwani haina bahari wala bandari.
Mzozo huo ulichukua sura mpya wakati Ethiopia ilipokataa kuhudhuria mkutano wa Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD ambayo ilikuwa imepanga kuongelea suala hilo. Ethiopia na Somalia ni wanachama wa IGAD.
Ethiopia ilitoa taarifa siku chache kabla ya mkutano huo wa marais wa nchi wanachama uliofanyika 17 Januari nchini Uganda, ikidai kuwa mkutano huo uliitishwa ndani ya muda mfupi na pia nchi hiyo ilikuwa na majukumu mengine siku hiyo ya mkutano.