Uganda inajenga uwanja mpya katika mji wa Hoima, mashariki mwa nchi / picha kutoka  @AFCONPAMOJA27

Baraza la Kitaifa la Michezo (NCS) limeomba bunge kuidhinisha zaidi ya dola milioni 101 ( Shilingi bilioni 379) kujiandaa kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu na Michezo, James Kubeketerya, wakati wa kuwasilisha taarifa ya Kamati ya Bajeti ya 2025/2026 kwa kikao cha bunge cha mapendekezo ya bajeti.

"Kamati inapendekeza kwamba Wizara ya Fedha itenge shilingi bilioni 379 kwa ajili ya maandalizi ya AFCON na shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya maandalizi ya timu ya taifa na mashindano makubwa ya kimataifa," alisema Kubeketerya.

Mnamo Septemba 2023, Shirikisho la Soka la Afrika lilitangaza Uganda, Kenya, na Tanzania kuwa waandaaji wenza wa AFCON ya 2027, yanayotarajiwa kufanyika kati ya Juni na Julai 2027.

Baraza hilo pia linaomba zaidi ya dola milioni 1.4 ( Shilingi bilioni 5.3) zaidi kusaidia maandalizi ya timu ya taifa Uganda Cranes kwa mashindano muhimu ya kimataifa.

Uganda tayari ina viwanja viwili, Namboole na Nakivubo katika mji mkuu, Kampala ambavyo viko karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe.

Uganda inajenga uwanja mpya katika mji wa Hoima, mashariki mwa nchi.

Uwanja huo unatakiwa kuwa na uwezo wa kuingia mashabiki 20,000.

TRT Afrika