Nchi 36 Afrika zina mkataba na Marekani chini ya mpango wa AGOA/ Picha: Reuters 

Eudes Ssekyondwa

TRT Afrika, Kampala, Uganda

Rais Museveni wa Uganda, amewataka wananchi wake "kutojali sana" hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Marekani ya kuiondoa Uganda katika mkataba wa biashara unaojulikana kama African Growth Opportunity Act, AGOA.

AGOA ilizinduliwa mwaka wa 2000, na Marekani kwa nia ya kuruhusu kuingiza bidhaa za Afrika katika soko la Marekani bila kulipia ushuru. Hii ilikuwa na nia ya kuinua nchi za Afrika kiuchumi huku zaidi ya bidhaa 1800 zikiwa katika orodha hiyo.

Lakini sasa Marekani imeamua kuiondoa Uganda katika mkataba huo kuanzia Januari 2024.

Hii inamaanisha kuwa wafanyabiashara kama Simon Musisi ambaye amekuwa akisafirisha Marekani tani 80 ya vanilla kila mwaka, bila kuzilipia ushuru, hataweza kuwa na fursa hiyo tena, itabidi aanze kulipa ushuru.

Katika kiwanda chake huko Entebbe, wafanyakazi wanapakia vanilla, mzigo wake wa mwisho kwenda Marekani mwaka huu.

Simon Musisi anauza tani 80 ya vanilla kila mwaka Marekani chini ya AGOA / Picha ya TRT Afrika

"Tulipata wateja nchini Marekani wanaonunua zaidi ya tani 60 za vanilla kutoka kwetu chini ya AGOA," anaiambia TRT Afrika.

"Sasa wateja wetu labda watalazimika kununua kwa gharama kubwa zaidi ikiwa bidhaa zitatozwa ushuru sasa," Musisi anaelezea TRT Afrika.

"Wale waliokuwa wakinunua kutoka kwetu watachagua kununua kutoka Madagascar, ambayo bado iko chini ya AGOA na mojawapo ya wauzaji wakubwa wa vanila duniani, hivyo tutaathirika sana."

Rais wa Marekani Joe Biden alisema katika barua ya bunge la Marekani kwamba "Serikali ya Uganda imehusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu zinazotambulika kimataifa."

AGOA ni chombo cha biashara au cha kuadhibu?

Mbali na Uganda Marekani pia imesimamisha mkataba na Gabon, Niger na Jamhuri ya Afrika ya kati.

Uganda imekosoa hatua ya Marekani kupiga marufuku mkataba wa kibiashara wa AGOA ikisema ilikuwa na lengo la "kuadhibu Uganda" kwa kupitisha sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja.

Uganda ilipitisha sheria hiyo Mei 2023

Odrek Rwabwogo, mshauri wa rais Yoweri Museveni anasema uamuzi huo wa Uganda haukuwa maarufu kwa rais Biden na wenzake.

"Inatuma ujumbe kwa wananchi wote wa Uganda - kwa hakika Waafrika wote - kwamba matarajio yao madogo ya ustawi wa kiuchumi yanategemea kama watapiga kura kulingana na maadili yatakayofikia nyadhifa za juu nchini Marekani, sio yao," Rwabogo alisema katika taarifa.

Chini ya AGOA makampuni ndani ya nchi za Afrika yanatengeneza nguo aina tofauti kwa ajili ya soko la Marekani / Picha: Reuters

Kando na baadhi ya bidhaa za kilimo, chini ya AGOA, Uganda imekuwa ikiuza Kahawa, pamba na nguo kwa soko la Marekani.

Kulingana na takwimu za Marekani, chini ya AGOA Marekani iliagiza kutoka Uganda bidhaa zenye thamani ya dola milioni 174 mwaka 2022.

Katika mwaka huo huo, mauzo ya bidhaa za Marekani kwenda Uganda yalikuwa na thamani ya dola milioni 167.

"Ikiwa Marekani inasimamisha Uganda katika soko lake basi AGOA itaumiza uchumi wetu kwa sababu tutakuwa tumekosa soko," Jane Nalunga, mtaalam wa biashara kutoka SEATINI anaimbia TRT Afrika, na kuongeza, "Tunahitaji masoko yote tuliyo nayo. Tunaweza kupata soko la Marekani, soko la EU au soko la Uchina."

Kwa ujumla, hata hivyo, hakuna usawa wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili. Takwimu za Marekani zinaonyesha kuwa mwaka 2023, kufikia Septemba, mauzo ya Marekani kwa Uganda yalikuwa na thamani ya $100.3M huku uagizaji kutoka Uganda ukiwa na thamani ya $97M.

Bidhaa nyingi zinazouzwa nje ya Uganda ni malighafi, hivyo huchota mapato kidogo tofauti na nchi ingeweza kupata iwapo bidhaa zingeongezewa thamani.

Bidhaa nyingi kutoka Afrika kwenda Marekani ni mali ghafi / Picha ya TRT Afrika

Rwabogo anasema mpango wa AGOA ulianzishwa kama "sera ya ukarimu mkubwa na kuona mbele kwa wale walioiunda ili kuifunga Afrika na Marekani katika ushirikiano na heshima."

"Haikuanzishwa kama kijiti cha kuwashinda wakazi wa nchi za Kiafrika wanaopiga kura kwa njia ambayo inakera hisia za jamii za Magharibi. Hata hivyo ndivyo, inavyotumika sasa,” anaongeza.

Marufuku ya biashara sasa inakuja baada ya uamuzi wa Benki ya Dunia mnamo Agosti 2023, kwamba hakutakuwa na ufadhili wa umma kwa Uganda kwa sababu "Sheria ya Kupinga Mapenzi ya Jinsia moja ya Uganda kimsingi inakinzana na maadili ya Kundi la Benki ya Dunia."

Nchi 36 Afrika zinaruhusiwa kutuma bidhaa zake Marekani chini ya AGOA.

Marekani imefungia nchi13 barani Afrika kutuma bidhaa nchini humo bila ushuru, ikitoa sababu tofauti kuwa hazifai/ Picha: Reuters 

Nchi nyengine zimeadhibiwa na Marekani kupitia AGOA pia.

Mwaka 2017 viongozi wa nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda walikubaliana kusitisha uingizaji wa nguo na viatu vya mitumba ifikapo mwaka 2019, kwa nia ya kusaidia viwanda vya ndani.

Marekani ilisema kuwa hii "haikuendana na vigezo vya manufaa ya AGOA" na hivyo basi, Rwanda ilisimamishwa kuingiza bidhaa nchini Marekani kwa siku 60.

Marekani imeorodhesha nchi 13 barani miongoni mwa nchi ambazo hazijafikia masharti ya kupata mkataba wa kutuma bidhaa katika soko la Marekani bila ushuru.

Hizi ni pamoja na Burundi, Cameroon, Equatorial Guinea, Eritrea, Ethiopia, Guinea, Mali, Mauritania, Seychelles, Somalia Sudan Kusini , Sudan na Zimbabwe.

Afrika inataka kuheshimiana katika biashara

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameutaja uamuzi wa Marekani kuwa wa kikatili.

"Shinikizo hili kutoka nje ni "joogo" ambayo ina maana ya kumdharau mtu, ni dharau kwa Waafrika na lazima zikataliwe," rais Museveni alisema.

Simon Musisi mfanyabiashara wa Vanilla Uganda. Picha/TRT Afrika

Museveni amekataa kushurutishwa kukubaliana na matakwa yote ya Marekani akisema, "Baadhi ya wahusika hawa katika Ulimwengu wa Magharibi wanajigamba kupita kiasi na kuwadharau wapigania uhuru wa Afrika."

"Kuhusu Uganda, tuna uwezo wa kufikia malengo yetu ya ukuaji na mabadiliko, hata kama baadhi ya wahusika hawatuungi mkono," Museveni ameongeza.

Afrika sasa inaelekeza umakini wake katika mpango wa biashara wa kibara, biashaŕa ya ndani ya Afrika, ambapo nchi 54 za Afrika zitafanya biashara zaidi baina yao.

Mataifa 47 ya Afrika hadi sasa yameidhinisha mpango wa bishara wa kibara ambao utalifanya bara la Afrika kuwa soko moja kubwa/ Picha ya TRT Afrika

Mpango huu unaitwa 'African Continental Free Trade Area,' (AfCFTA) na mkataba wake ulikubaliwa na viongozi wa serikali za Afrika mwaka 2018.

"Bara la Afrika limepiga hatua katika kutengeneza soko la ndani linaloanzisha kanuni za ushirikiano wa kiuchumi," Wamkele Mene, katibu Mtendaji wa ACFTA aliliambia Kongamano la AGOA la 2023 lililofanyika Afrika Kusini kuanzia tarehe 4 hadi 9 Novemba.

"Hiyo ina maana kwamba inatubidi kufikiria AGOA katika muktadha huu mpya uliowasilishwa na AfCFTA."

Lengo lake ni kuondoa vikwazo vya biashara barani na kupanua biashara ndani ya Afrika. Itatoa soko la takribani watu bilioni 1.3 ambayo ndiyo idadi wa nchi 54 za Afrika.

Mataifa 47 ya Afrika hadi sasa yameidhinisha mpango huo wa AfCFTA na juhudi zinaendelea kuhakikisha unatekelezwa kikamilifu.

"Lazima tuhakikishe kuwa, AGOA chini ya Marekani inaunga mkono utekelezaji wa AfCFTA na kwamba AGOA haidhoofishi maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi ambayo Afrika imefikia kupitia AfCFTA. Bara letu linatafuta usawa kati ya Afrika na mataifa mengine ya magharibi."

"Hizi zinapaswa kuwa siku ambazo Afrika haionekani tu kama chanzo cha miamba, ardhi, na rasilimali asili na vumbi linalosafirishwa nje ya bara letu," Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alisema wakati wa mkutano wa AGOA la 2023.

"Sasa tunataka kuzalisha bidhaa iliyokamilika au iliyokaribia kukamilika ambayo inatumika katika sehemu nyingine za dunia. Tunataka kupata thamani kamili ya bidhaa zetu," Ramaphosa aliongezea.

Mazungumzo kati ya nchi wanachama wa Afrika yanaendelea ili kubaini ukweli wa biashara ndani ya Afrika bila vikwazo vyovyote vya kibiashara.

Na wakati AU inaharakisha mchakato huu wa kibara, wafanyabiashara kama Musisi nchini Uganda tayari wanatafuta masoko mbadala kwa sababu, kuanzia Januari 2024, Marekani bila ushuru hautakuwepo tena.

TRT Afrika