Polisi wa Kenya waliokuwa wamevalia sare na bila vitambulisho rasmi waliwafyatulia risasi waandamanaji katika majengo ya bunge la nchi hiyo mjini Nairobi mnamo Juni 25, shirika la Amnesty International lilisema Jumatano.
''Siku hiyo ilishuhudia matumizi ya maafisa wasio na vitambulisho, sare au magari yaliyowekwa alama kama magari ya polisi yakiwapiga risasi waandamanaji na kuwakamata wengine," alisema Irũngũ Houghton, mkurugenzi wa Amnesty Kenya.
Wakati wa uzinduzi wa ripoti yao kwa wanahabari, Amnesty, ikishirikiana na mashirika sita ya haki za binadamu, mashirika ya sheria na ile ya matabibu, pamoja na Chama cha Wanasheria cha Kenya, ilisema kuwa kulikuwa na ukiukaji wa wazi wa sheria na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na Kanuni za Msingi za Umoja wa Mataifa juu ya Matumizi ya Nguvu na Silaha kwa Maafisa wa Utekelezaji wa Sheria.
“Haki ya kuandamana nchini Kenya inalindwa chini ya katiba. Haikubaliki kwamba, badala ya kuwezesha na kuwalinda waandamanaji, polisi waliamua kutumia nguvu mbaya,” alisema Irũngũ.
Ripoti hiyo pia inashutumu polisi wa kukabiliana na ghasia kutumia silaha zisizoua kama vile mabomu ya kuto amachozi, maji ya kuwasha na fimbo, kuwapiga wahudumu wa afya waliokuwa wakitoa huduma ya dharura, pamoja na waandishi wa habari.
GenZ wakataa kurudi nyuma
Mnamo tarehe 25 Juni, miezi mitatu iliyopita, maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika wilaya ya kati ya biashara ya Nairobi na kaunti zingine kote nchini kupinga mswada wa fedha uliopendekeza kuongezeka kwa ushuru, ikijumuisha hatua za kupunguza ushuru huku kukiwa na gharama kubwa ya maisha.
Maandamano hayo yaliendelea kwa wiki kadhaa, licha ya Rais kutangaza kuwa amerudisha mswada huo ukajadiliwe upya bungeni, na kuridhia baadhi ya mapendekezo ya waandamanaji hao, kama vile kuvunja baraza la mawaziri.
Rais hata hivyo aliwarudisha kazi wengi wa mawaziri aliokuwa amewafuta japo kwa kuwahamisha wizara.
Wakusanya saini 12000
Watu 12,00O wametia saini ombi la Amnesty International la kutaka kuundwe Tume ya mahakama ya Uchunguzi na uwajibikaji kwa vifo na majeraha yanayotokana na matumizi ya polisi kinyume cha sheria dhidi ya waandamanaji nchini Kenya.
Kufikia mwisho wa Agosti, Chama cha Wanasheria nchini Kenya kilikuwa kimerekodi watu 72 ambao walikuwa wametekwa nyara, kuachiliwa au walikuwa bado hawajapatikana kuhusiana na maandamano hayo. Kumi na tatu walitoweka tarehe 25 Juni na wengine ishirini na watatu walitoweka ndani ya siku saba za maandamano hayo.
Takriban watu 61 waliuawa wakati polisi wakitawanya maandamano hayo yaliyofuatiliwa na wengi nje na ndani ya Afrika.