Watu watatu wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha ndege ndogo iliyoanguka katika eneo la Kwachocha huko Malindi, Kaunti ya Kilifi, siku ya Januari 10.
Inasemekana kuwa, ndege hiyo aina ya Cessna 172 ya Chuo cha Kenya Aeronautical College, ilipata hitilafu ya kiufundi na kulazimika kutua kwenye barabara kuu ya Malindi-Mombasa, kabla haijashika moto na kusababisha vifo vya watu watatu, wakiwemo mwalimu mmoja na waendesha bodaboda wawili.
Kulingana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya (KCAA), ndege hiyo yenye namba za usajili 5Y-CDC, ilianguka takribani kilomita mibili kutoka uwanja wa ndege wa Malindi na kushika moto.
Ndege hiyo ya mafunzo ilikuwa na abiria 3 ambao walikimbizwa hospitali mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo.
Tayari, KCAA imeanza uchunguzi wa tukio hilo.