Wanawake wanne kati ya 10 au wastani wa 41% ya wanawake waliochumbiwa au walioolewa wamepitia ukatili wa kimwili au kingono./ Picha: Reuters 

Mahali hatari zaidi kwa wanawake ni nyumbani, huku wanawake na wasichana 140 kwa wastani wakiuawa na wapenzi wao wa karibu au mwanafamilia kwa siku mwaka jana, mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yaliripoti Jumatatu.

Idadi kubwa zaidi ya mauaji yanayofanywa na watu wa karibu na familia ilikuwa barani Afrika - na wastani wa waathiriwa 21,700 mnamo 2023, ripoti ilisema.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na UN Women na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Afrika pia ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya waathiriwa ikilinganishwa na idadi ya watu wake - waathiriwa 3 kwa kila watu 100,000.

Ripoti hiyo iliyotolewa katika Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake imesema ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na takwimu nyingi zaidi kutoka katika mataifa na sio kuwa mauaji yameongezeka.

Ukatili dhidi ya wanawake waripotiwa kila siku

"Wanawake na wasichana kila mahali wanaendelea kuathiriwa na aina hii ya ukatili wa kijinsia na hakuna eneo ambalo limetengwa." ilisema ripot hiyo. "Nyumbani ni mahali hatari zaidi kwa wanawake na wasichana." iliongeza kusema.

Hii inakuja wakati mwaka 2024, kumekuwa na ongezeko kubwa la mauaji ya wanawake yanayolaumiwa wapenzi wao wa karibu au wanafamilia nchini Kenya.

Kisa cha punde zaidi ni Novemba 21 ambapo mwanamume mmoja anatuhumiwa kumvamia mume wake na kumchoma kisu mara 18 mwilini.

Elias Njeru, ambaye ni mkuu wa kanisa na mfanyabiashara mjini Nakuru, mkoa wa Rift Valley, anakabiliwa na shtaka la jaribio la mauaji ya Florence Wanjiku Gichohi. Elias amejisalimisha Jumatatu kwa kituo cha polisi akiwa na wakili wake.

Mnamo Septemba 2024, mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei aliuawa na mpenzi wake nchini Kenya, akiwa mwanariadha wa nne wa kike kuuawa na mpenzi wake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Shirika la habari la uchunguzi, Africa Uncensored, linakadiria kuwa wanawake 500 waliuawa nchini Kenya kati ya 2017 na 2024. Shirika la Femicide Count, nchini Kenya, lilirekodi visa 152 vya mauaji ya wanawake mwaka wa 2023 kulingana na ripoti za vyombo vya habari.

Serikali ya Kenya imeelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia (GBV) na kesi za mauaji ya wanawake.

Rais Willliam Ruto ametoa Ksh100 milioni kwa kampeni ya uhamasishaji dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Na kwa mujibu wa utafiti wa Demografia na Afya wa Kenya wa 2022. Wanawake wanne kati ya 10 au wastani wa 41% ya wanawake waliochumbiwa au walioolewa wamepitia ukatili wa kimwili au kingono unaofanywa na wapenzi wao wa sasa au waliotangulia.

Hali inalingana vipi nje ya Afrika?

Lakini mashirika hayo mawili yalisisitiza kuwa "Wanawake na wasichana kila mahali wanaendelea kuathiriwa na aina hii ya ukatili wa kijinsia na hakuna eneo ambalo limetengwa.

Kulingana na UN Women, kulikuwa na viwango vya juu mwaka jana katika Amerika na waathiriwa wa kike 1.6 kwa 100,000 na Oceania na 1.5 kwa 100,000, ilisema. Viwango vilikuwa vya chini sana barani Asia kwa waathiriwa 0.8 kwa 100,000 na Ulaya kwa 0.6 kwa 100,000.

''Ulimwenguni kote, mshirika wa karibu au mwanafamilia alihusika na vifo vya takriban wanawake na wasichana 51,100 wakati wa 2023, ongezeko kutoka kwa wastani wa waathiriwa 48,800 mnamo 2022.'' ilisema ripoti.

TRT Afrika