"Ugonjwa ambao haukujulikana hapo awali ambao umeuwa makumi ya watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC huenda ukawa malaria, Shirika la Afya la Umoja wa Afrika," Africa CDC ilisema Alhamisi.
Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Oktoba, ambapo maambukizi yaliripotiwa katika eneo la Panzi, takriban kilomita 700 kusini mashariki mwa mji mkuu, Kinshasa.
"Utambuzi wa sasa ni kuwa ni ugonjwa wa malaria," Ngashi Ngongo, Mkuu wa wafanyakazi wa Afrika CDC na Mkuu wa ofisi ya utendaji aliuambia mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandaoni.
"Hali hiyo imechangiwa na utapiamlo katika eneo hilo," alisema, akielezea kuwa dhana ya ugonjwa huo kuwa malaria inawezekana zaidi.
Ngongo amesema uwezekano wa kuwa ugonjwa wa virusi vya kuvuja damu bado haijafutiliwa mbali.
Ugonjwa huo umewauwa watu 37 katika vituo vya afya huko Panzi ikiwa na takriban wagonjwa 600, takwimu kutoka Africa CDC zilionyesha.
Baadhi ya vifo vyengine 44 vimeripotiwa katika ngazi ya jamii na vilikuwa chini ya uchunguzi.
Ufikiaji wa mkoa huo ni mgumu kwa barabara na miundombinu ya afya inakosekana. Wakazi pia wanakabiliwa na uhaba wa maji ya kunywa na dawa.
Kulingana na mamlaka ya Congo, eneo hilo, ambalo lilikumbwa na janga la homa ya matumbo miaka miwili iliyopita, lina moja ya viwango vya juu zaidi vya utapiamlo nchini kwa 61%.
Mapema mwezi huu, wataalam wa magonjwa ya mlipuko waliondoa uwezekano wa 'coronavirus' lakini walihitimisha kuwa ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa kupumua.
Dalili zake ni pamoja na homa, kikohozi na maumivu ya kichwa.
Takwimu za awali zilionyesha kuwa ugonjwa huo uliwaathiri zaidi vijana, na 40% ya maambukizi yanazohusisha watoto chini ya miaka mitano.
DRC, katika miezi ya hivi karibuni imekuwa kwenye kitovu cha mlipuko wa ugonjwa wa Mpox, na vifo vya zaidi ya 1,000.