Na Susan Mwongeli
TRT Afrika, Adana, Uturuki
Teknofest, maonyesho makubwa zaidi ya teknolojia na anga ya Uturuki, yalihitimishwa huko Adana, na kuashiria toleo jingine lililofaulu.
Tukio la kila mwaka, linalofanyika katika miji tofauti ya Uturuki, linaonyesha maendeleo ya hivi punde katika sekta ya teknolojia, haswa katika anga na akili mnemba.
Mwaka huu pia haukuwa tofauti, kwani wapenda teknolojia wa kimataifa walikusanyika ili kujionea ubunifu wa Uturuki.
Teknolojia kadhaa za kisasa zilizinduliwa, ikiwa ni pamoja na gari la umeme la Togg, T1OF, na ndege isiyo na rubani ya Baykar, Bayraktar TB3, ambayo ilianza kuonyeshwa hadharani pamoja na Bayraktar Akinci UAV.
Miongoni mwa waliohudhuria kimataifa walikuwa wanafunzi wa Kiafrika, ambao walisifu maendeleo ya teknolojia ya Uturuki.
"Teknofest ni fursa nzuri kwa wanafunzi, hasa wale wanaopenda teknolojia, kwani Uturuki inashinda katika teknolojia ya ndege zisizo na rubani na ndege," alisema Lyvan Tebri, mwanafunzi kutoka Côte d'Ivoire.
Racha Badreddinean, mwanafunzi wa chuo kikuu wa Algeria huko Uturuki, aliangazia fursa muhimu za Teknofest.
"Kama Mwafrika, kushiriki katika hafla hii ya kimataifa ni fursa nzuri ya kujifunza na kugundua teknolojia zilizotengenezwa na nchi zingine," aliiambia TRT Afrika.
Badreddinean alibainisha kuwa fursa ya kuingiliana na wataalamu kutoka sekta mbali mbali na kuhudhuria maonyesho ya Teknofest zinaongeza uwezo wake wa kuchangia maendeleo ya nchi yake na bara kwa ujumla.
Teknofest 2024 iliangazia mashindano, huku washiriki wabunifu wakipokea zawadi.
Timu ya Chuo Kikuu cha Istanbul Arel ilishinda tuzo ya kwanza na mradi wao "Warscope," programu ya mtandaoni inayotiririsha takwimu za vita kwa wakati halisi yaani papo hapo.
"Hatujalala kwa siku mbili, lakini kila wakati ulikuwa wa thamani," alisema Hasan İnan, mwanachama wa timu iliyoshinda.
Imeandaliwa kwa pamoja na Wakfu wa Timu ya Teknolojia ya Uturuki na Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Jamhuri ya Uturuki, Teknofest imeipa kipao mbele maendeleo ya teknolojia tangu 2018.
Mnamo 2025, Teknofest itafanyika mara mbili, katika Jamhuri ya Uturuki ya Kupro ya Kaskazini na Istanbul, alisema Selcuk Bayraktar, mkuu wa mratibu wa hafla, Wakfu wa Timu ya Teknolojia ya Uturuki.
"Katika tamasha za mwakani, tutapata mafanikio mapya pamoja na vijana wa nchi yetu na wa kutoka kwenye eneo lenye na urafiki na Uturuki."