Uturuki inategemea utekelezwaji wa haraka wa maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya kuitaka Israeli kusitisha mashambulizi yake katika mji wa Rafah.
"Hakuna nchi iliyo juu ya sheria duniani. Ni mategemeo yetu kuwa maamuzi yote ya Mahakama hiyo yatatekelezwa kikamilifu na Israeli. Hili litafanikiwa ikiwa tu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litatimiza wajibu wake," ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki katika taarifa yake ya Ijumaa.
Hapo awali, mahakama hiyo ya kimataifa iliiamuru Israeli kusitisha mashumbulizi yake katika mji wa Rafah na kufungua kivuko cha Rafah, ili kufanikisha mchakato wa upatikanaji wa taarifa muhimu katika eneo hilo.
Katika taarifa nyingine, Waziri wa Sheria wa Uturuki Yilmaz Tunc amesema uamuzi wa ICJ ni wa "muhimu lakini hautoshi kumaliza umwagaji damu na machozi ya Wapalestina."
"Ni lazima Israeli iache kufanya kazi kama shirika la kigaidi na kutimiza matakwa ya sheria za kimataifa," alisema na kuongeza kuwa "nchi na mashirika ya kimataifa ambayo yanaamini katika demokrasia na haki za binadamu yanapaswa pia kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa Israeli inazingatia maamuzi."
Tunc alisisitiza zaidi kwamba Uturuki itaendelea kusimama pamoja na watu wasio na hatia wa Palestina katika haki yao, kuiwajibisha Israeli dhidi ya jumuiya ya kimataifa ili kuhakikisha kwamba usitishaji vita unatangazwa na maafisa wa Israeli wanaadhibiwa kwa ukatili wao ambao ni sawa na mauaji ya halaiki.
Rafah: Njia kuu ya kufikisha misaada
Israel imeendeleza mashambulizi yake makali dhidi ya Gaza tangu Oktoba 7, 2023, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika eneo hilo.
Zaidi ya miezi saba ya vita vya Israel, maeneo makubwa ya Gaza yamegeuka kuwa magofu huku kukiwa na vizuizi vya upatikanaji wa chakula, maji safi na dawa.
Takriban Wapalestina 35,800 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine zaidi ya 80,200 wamejeruhiwa tangu Oktoba mwaka jana kufuatia shambulio la kuvuka mpaka la kundi la Palestina la Hamas.
Israeli ilishambulia mji wa kusini wa Rafah mwezi huu, na kuwalazimu mamia kwa maelfu ya Wapalestina kuukimbia mji ambao umekuwa kimbilio la karibu nusu ya watu milioni 2.3 wa wakaazi hao.
Rafah, iliyo katika ukingo wa kusini wa Gaza, pia imekuwa njia kuu ya uingizaji wa misaada, na mashirika ya kimataifa yanasema operesheni ya Israeli inaongeza hatari ya njaa.
Hatua za dharura
Maamuzi dhidi ya Israeli yataongeza shinikizo zaidi la kidiplomasia kwa serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - mahakama tofauti ambayo pia iko The Hague - alitangaza Jumatatu kuwa amewasilisha ombi la kukamatwa kwa Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, pamoja na viongozi wa Hamas.
Karim Khan alimshutumu Netanyahu na Gallant kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na kuwaangamiza watu, kutumia njaa kama silaha na kushambulia raia kwa makusudi . Israeli ilikanusha vikali mashtaka hayo na kuwataka washirika kuikataa mahakama hiyo.
Afrika Kusini imefungua kesi katika mahakama ya ICJ, ikiituhumu Israeli kwa kupanga mauaji ya kimbari yanayoongozwa na serikali dhidi ya watu wa Palestina.
ICJ haijatoa uamuzi juu ya kiini cha mashtaka hayo - jambo ambalo linaweza kuchukua miaka - lakini imekataa ombi la Israeli la kutupilia mbali kesi hiyo.