Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun amelishtumu jarida la 'The Economist', akilaumu jarida hilo kwa kupotosha ukweli kuhusu kesi zinazoendelea mahakamani nchini Uturuki na kumlenga Rais Recep Tayyip Erdogan.
"Jarida la 'The Economist' linathubutu kumshtumu Rais wetu Recep Tayyip Erdogan kwa kupotosha ukweli kuhusu baadhi ya kesi na uchunguzi unaoendeshwa na mahakama huru za Uturuki. Ni jarida hilo hilo ambalo limekaa kimya kwa miezi kadhaa wakati Israeli ikiendeleza mauaji ya halaiki na ukatili wake huko Gaza sasa linajaribu eti kutusema sisi," Altun alisema katika ujumbe aliouweka kwenye mtandao wake rasmi wa X siku ya Jumapili
Aliongeza, "Hatuna cha kujifunza kutoka jarida hilo, ambalo linakiuka utaratibu wa sheria ulimwenguni, linaunga mkono Israeli moja kwa moja bila kuhoji, na kujaribu kuwanyamazisha wale wanaounga mkono haki za watu wa Wapalestina waliokandamizwa. Lakini lazima tuchukue tahadhari."
Dhamira ya Uturuki
Altun pia alitaja kile alichokieleza kuwa njama iliyopangwa kuharibu sifa ya Uturuki ambayo imepata mafanikio makubwa katika sekta ya televisheni duniani. "Njama hii, ambayo inalenga Televisheni za Uturuki zenye mafanikio kimataifa, ni sehemu ya mpango ulioandaliwa kuweka msingi wa njama kubwa zaidi. Si chochote isipokuwa ni njama mpya ya dunia dhidi ya Uturuki."
Alisisitiza dhamira ya Uturuki kuangazia malengo yake ya maendeleo, akisema: "Kwa vyovyote vile, chini ya uongozi wa Rais wetu, tutaendelea na juhudi zetu za kuwa na Uturuki yenye uwezo na mafanikio zaidi bila kutatizwa na njama zao mbaya."
Altun alikamilisha taarifa yake kwa kueleza wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma. "Mwisho, tumeona raslimali za umma za baadhi ya mabaraza ya miji yetu zikitumiwa kwa masuala haya ya kujitafutia umaarufu ambayo hayana msingi. Tuachie taifa letu lifanye maamuzi kuhusu hili," alisema.