"Israel imekuwa ikifanya ukatili huu kwa muda mrefu. Imeweza kufanya hivi kwa sababu hakuna upinzani mkali kutoka kwa ulimwengu wa Magharibi," Altun alisema. / Picha: AA  

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun amelaani vikali mashambulizi ya Israel yaliyolenga wanahabari kufuatia shambulio kwenye kambi ya Nuseirat huko Gaza ya Palestina, ambalo lilijeruhi waandishi kadhaa wa habari wakiwemo wale wa idhaa ya TRT Arabi.

"Hata iweje, tutaendelea kuueleza ulimwengu kuhusu ukatili wa Israel dhidi ya raia," Altun alisema katika mahojiano na TRT kufuatia shambulio la Ijumaa mchana.

Alisisitiza kuwa Tel Aviv pia inapigana vita dhidi ya ukweli kwa "makusudi, kwa makusudi kulenga" waandishi wa habari walioko kazini.

Israel inapigana vita dhidi ya ukweli kwa "kukusudia, kulenga" waandishi wa habari, anasema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Uturuki Altun kufuatia shambulizi la kifaru lililojeruhi wanahabari kadhaa wakiwemo wale wa kituo cha TRT Arabi.

"Israel imekuwa ikifanya ukatili huu kwa muda mrefu. Imeweza kufanya hivi kwa sababu hakuna upinzani mkali kutoka kwa ulimwengu wa Magharibi," aliongeza.

Mpigapicha wa TRT Sami Shehadeh, ambaye ni sehemu ya wafanyakazi wanaoripoti kutoka kambi ya wakimbizi katikati mwa Gaza, alijeruhiwa vibaya na kupoteza mguu wake kufuatia shambulizi la kifaru la Israel, siku ya Ijumaa.

Mwakilishi wa TRT Arabi Sami Berhum pamoja na waandishi wa habari wengine pia walijeruhiwa katika tukio hilo. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, jeshi la Israel lililenga kundi la waandishi wa habari kwa makusudi.

Mkurugenzi Mkuu wa TRT, Zahid Sobaci alilaani shambulio hilo, na kulielezea kama "ukatili" usio na "kikomo cha maadili, kisheria au kibinadamu."

Naibu Mwenyekiti wa Chama cha AK na Msemaji wa Chama Omer Celik pia alilaani shambulizi lililolengwa na kutuma salamu zao za heri kwa wanahabari.

"Kwa mara nyingine tena, tunalaani jeshi la Israel, ambalo linawaua kikatili Wapalestina huko Gaza, kwa kuwalenga waandishi wa habari ambao wanaleta hali ya kibinadamu katika eneo hilo kwenye ajenda ya ulimwengu," aliandika kwenye ukurasa wa X.

Hii si ni mara ya kwanza kwa jeshi la Israel kuwalenga waandishi wa habari huko Gaza wakati wa vita vyake vinavyoendelea kwa zaidi ya nusu mwaka. Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Gaza, waandishi wa habari wasiopungua 140 wamepoteza maisha katika mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Jana, jeshi la Israel lilitangaza kuanza kwa "operesheni ya kushtukiza" katikati mwa Gaza, ambayo ilisababisha mauaji ya Wapalestina wengi.

Vita vya Israel dhidi ya Wapalestina vimefikia siku ya 189, na kusababisha vifo vya Wapalestina 33,545 na wengine 76,094 kujeruhiwa.

TRT Afrika