Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki

Uturuki iko katika mazungumzo na pande zote mbili nchini Sudan kwa ajili ya kusitisha mapigano, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amesema.

“Pande zote mbili ni ndugu zetu wa Sudan. Kwa nini tuchukue upande hapa? Tunafanya mazungumzo na pande zote mbili.

Tunafanya mazungumzo ya kusitisha mzozo huo,” Mevlut Cavusoglu alisema katika hafla katika jimbo la Antalya la Uturuki siku ya Jumatano.

Cavusoglu alisema anatarajia usitishaji mapigano kufikiwa siku ya Alhamisi.

Aidha alisema raia wa Uturuki wanaotaka kurejea nchini mwao watahamishwa kutoka Sudan wakati anga itafunguliwa siku ya Alhamisi.

Alisema nchi nyingi zikiwemo za Ulaya zimeomba usaidizi kutoka Uturuki ili kuwahamisha raia wao kutoka Sudan.

Mapigano yaliendelea kwa siku ya 5 kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko Khartoum na maeneo yanayozunguka, na kusababisha vifo vya takriban 270 na wengine 2,600 kujeruhiwa, kulingana na Wizara ya Afya.

TRT Afrika