Fahrettin Altun anasisitiza wito wa Rais Erdogan wa mageuzi katika utawala wa kimataifa, akitetea mfumo wa usawa zaidi wa kushughulikia masuala ya dharura kama mzozo wa Palestina. / Picha: AA

Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki Fahrettin Altun amethibitisha jukumu muhimu la Ankara katika kutatua mzozo wa Syria na kushughulikia kukosekana kwa utulivu wa kikanda huku akikosoa vikali unafiki wa nchi za Magharibi na upendeleo wa vyombo vya habari juu ya mzozo unaoendelea huko Gaza, Palestina.

Altun alielezea juhudi za Uturuki kukuza amani nchini Syria na kulaani kwake kutochukuliwa hatua kimataifa juu ya mateso ya Wapalestina, amesema hayo katika mahojiano ya kina na chapisho la Kituruki.

Alisisitiza msimamo wa Uturuki kama mhusika mkuu wa kikanda katika kutafuta suluhu la kina la mzozo wa muda mrefu wa Syria.

Akiangazia kuwa Rais Recep Tayyip Erdogan yuko tayari kuwasiliana na kiongozi wa serikali ya Syria Bashar al Assad, Altun alisema mazungumzo hayo ni muhimu huku kukiwa na ongezeko la ghasia, uchokozi na watu wengi kuhama makazi yao.

"Tumedhamiria kuendeleza mchakato unaozingatia kanuni za kupambana na ugaidi ili kuhakikisha uhalali wa ardhi ya Syria, kuendeleza mchakato wa kisiasa ulioanzishwa kwenye Azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa chini ya umiliki wa Syria, na kuweka mazingira yanayofaa kurudi kwa Wasyria kwa njia ya usalama na kwa hiari," alisema.

Altun alisisitiza kwamba kanuni hizi zinalenga kushughulikia sababu kuu za matatizo ya Syria. Aliongeza kusema kuwa ushirikiano wowote,lazima pia uwezeshe mazungumzo ya kweli kati ya vyama vya Syria, kama ilivyoainishwa na maazimio husika ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Uturuki imedumisha dhamira yake ya kupambana na ugaidi, kuhakikisha usalama wa watu waliokimbia makazi yao, na kuhimiza amani katika eneo hilo. "Uturuki inafaidika na azimio la amani nchini Syria, na tumejitolea kikamilifu kwa mchakato huu," Altun alisema.

Udhalimu wa Gaza

Akigeukia vita vinavyoendelea vya Israeli huko Gaza, Altun alilaani maafa ya kibinadamu na kuzishutumu serikali za Magharibi na vyombo vya habari kwa upendeleo wa wazi.

Alitaja taswira ya vyombo vya habari kuhusu uvamizi wa Israeli kuwa ni jaribio la makusudi la kupotosha ukweli na kuwadhalilisha Wapalestina.

"Tangu Oktoba 7, imedhihirika kuwa maadili ya Kimagharibi kama vile haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari yanatumika tu kwa watu wachache waliobahatika wanaohusishwa na mtazamo wa ulimwengu wa Magharibi," Altun alisema.

Aliangazia udhibiti na unyanyasaji unaowakabili waandishi wa habari wa Magharibi na wasomi ambao walionyesha maoni tofauti, akiita "mfano dhahiri wa unafiki."

"Hali hii ya upendeleo haikubaliani na ukandamizaji tu bali pia inaiwezesha kikamilifu," aliongeza.

Altun alishtumu zaidi Israeli kwa kutumia habari za uwongo ili kuhalalisha vitendo vyake.

Alirejelea madai ya uwongo ya Rais wa Israeli Isaac Herzog katika Mkutano wa Usalama wa Munich, ambapo Herzog alidai kuwa kitabu kilichopatikana Gaza kilichochea mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi.

Kituo cha Taarifa za Kupambana na habari potofu cha Uturuki kilifichua madai hayo kama uzushi, kuonyesha kwamba kitabu hicho, kilichoandikwa nchini Misri katika miaka ya 1990, hakikuwa na uhusiano wowote na Palestina au Hamas.

"Uongo huu wa makusudi, uliosambazwa kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, ulilenga kugeuza ukweli na kuwaonyesha Wapalestina kama wahusika wa mauaji ya halaiki," Altun alieleza.

Wito wa mageuzi ya kimataifa

Altun alisisitiza wito wa Rais Erdogan wa mageuzi katika utawala wa kimataifa, akitetea kuwepo kwa mfumo wa usawa zaidi wa kushughulikia masuala ya dharura kama vile uvamizi wa Israeli katika maeneo ya Palestina.

"Mfumo wa sasa wa kimataifa unalinda maslahi ya wenye nguvu, na kuacha masuala mengi muhimu bila kutatuliwa. Hii ndiyo sababu msimamo wa Rais Erdoğan, 'Dunia ni kubwa kuliko tano,' inasikika zaidi kuliko hapo awali," alisema.

Altun alisisitiza jukumu kubwa la Uturuki katika vikao kama vile G20, ambayo alielezea kama majukwaa muhimu ya kushughulikia changamoto zilizounganishwa za kimataifa kama vile usalama wa chakula, uhamiaji, na mabadiliko ya hali ya hewa."Kama kawaida, Uturuki itatekeleza majukumu yake, ikifanya kazi kupitia taasisi zenye ufanisi kama G20 kuleta utulivu katika mfumo wa kimataifa unaozidi kuwa dhaifu," alihitimisha.

TRT World