Uturuki inakataa pendekezo la Trump la kuwafukuza Wapalestina kutoka Gaza - Fidan

Uturuki inakataa pendekezo la Trump la kuwafukuza Wapalestina kutoka Gaza - Fidan

Pendekezo linakwenda kinyume na sheria za kibinadamu, asema waziri wa mambo ya nje wa Uturuki.
Fidan amesema kuwa Uturuki inaweza kuwachukua baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru na Israeli chini ya masharti ya mkataba wake wa kusitisha mapigano na Hamas. / Picha: AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema Ankara "inapinga kabisa" pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuwafukuza Wapalestina kutoka Gaza na kuwapeleka katika nchi nyingine.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa wanahabari siku ya Jumapili na mwenzake wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, mjini Doha, Fidan amesema pendekezo hilo linakwenda kinyume na sheria za kibinadamu.

Amesisitiza kuwa kila mtu anapaswa kuupinga mpango huo na kuongeza kuwa, Ankara inaunga mkono azimio la hivi karibuni lililotolewa mjini Cairo kuhusu Wapalestina huko Gaza.

Fidan pia alisema kuwa Uturuki inaweza kuwachukua baadhi ya wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru na Israeli chini ya masharti ya mkataba wake wa kusitisha mapigano na Hamas.

"Rais wetu ametangaza kuwa tuko tayari kuchukua baadhi ya Wapalestina walioachiliwa huru... ili kuunga mkono makubaliano hayo.

Uturuki, pamoja na nchi nyingine, zitachukua nafasi yake katika suala hili ili makubaliano ya kusitisha mapigano yaendelee kutekelezwa," alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Doha.

Fidan yuko katika ziara ya siku mbili nchini Qatar ilioanza Jumapili.

TRT World