Uturuki haitaruhusu siasa zake kuongozwa na majarida, Rais Recep Tayyip Erdogan amesema.
"Hatutaruhusu siasa zetu za ndani na nia ya kitaifa kuyumbishwa na majarida, ambayo ni vyombo vya uendeshaji wa mataifa yenye nguvu duniani," Erdogan alisema Ijumaa kupitia Twitter.
Matamshi ya Erdogan yalikuja baada ya jarida la Uingereza la The Economist kumlenga rais wa Uturuki kwa jalada lililosema "Okoa demokrasia," "Erdogan lazima aende," "Piga kura!" Mjini Uturuki, uchaguzi wa rais na bunge utafanyika Mei 14.
Kwenye kura ya urais, wapiga kura watachagua kati ya Erdogan, ambaye anawania kuchaguliwa tena, na wagombea wakuu wa upinzani Kemal Kilicdaroglu, Muharrem Ince, na Sinan Ogan.
Wakati huo huo, vyama 24 vya kisiasa na wagombea binafsi 151 wanachuana kuwania viti katika bunge la Uturuki lenye wabunge 600.
Sera ya 'kujiamini'
Kuhusu sera ya kigeni ya Uturuki, rais alisema kwa juhudi za wanadiplomasia wa Uturuki, nchi hiyo imetekeleza sera ya "kujiamini, ujasiriamali na kibinadamu".
“Kwa kuongeza idadi ya wawakilishi wetu wa kigeni kutoka 163 hadi 260, tumekuwa miongoni mwa nchi tano zenye mtandao mkubwa wa kidiplomasia duniani,” aliongeza.
Uturuki inasimama na ndugu kwa uwezo wetu wote inapobidi, kama vile Libya, Syria, na Karabakh, ambayo ilikombolewa baada ya miaka 30 ya uvamizi wa Armenia, Erdogan alisisitiza, akiongeza kwamba Ankara inachangia ufumbuzi wa migogoro ya kikanda kupitia mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi.
“Kama taifa ambalo historia yake imejaa ushindi mnono, tunafika mahali tunapostahili katika mfumo wa kimataifa. "... Tunatumai, kwa Karne ya Uturuki, tutabeba mafanikio haya yote ya kidiplomasia hadi juu," Erdogan aliongeza.