Ukraine inataka Uturuki iwe sehemu ya mazungumzo ya amani, Zelensky amwambia Erdogan

Ukraine inataka Uturuki iwe sehemu ya mazungumzo ya amani, Zelensky amwambia Erdogan

Kulingana na Volodymyr Zelensky, hakuna maamuzi yoyote yatakayofikiwa bila ushrikishwaji wa moja kwa moja wa Kiev.
Recep Tayyip Erdogan

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa uhakika wa nchi yake kuisadia Ukraine iweze kujitawala, huku ikisema kuwa Ankara iko tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya Ukraine, Urusi na Marekani.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari akiwa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy siku ya Jumanne jijini Ankara, viongozi hao wamekosoa hatua ya kuondolewa kwa Ukraine, mataifa ya Ulaya na Uturuki katika mazungumzo ya amani ya hivi karibuni kati ya Marekani na Urusi yaliyofanyika Riyadh, akisisitiza kuwa hakuna maazimio yatakayofikiwa bila ushirikishwaji wa moja kwa moja wa Kiev.

"Uturuki imekuwa na msimamo thabiti kwenye suala la haki ya kujitawala la Ukraine,"alisema Zelenskyy, akiishukuru Ankara kwa jitihada zake za kufanikisha kuachiwa huru kwa wanajeshi wa Ukraine na raia.

Kulingana na Zelenskyy, ni lazima Ukraine na Uturuki ziwe sehemu ya mazungumzo ya amani na Urusi.

Akionesha msimamo wa Uturuki, Erdogan alisema kuwa Ankara itaendelea kuunga mkono majadiliano hayo ili kupata amani ya kudumu.

"Vita hivi vimesababisha vifo vingi na uharibifu mkubwa, ni lazima vimalizike," alisema.

Alisisitiza kuwa Uturuki itatoa kila aina ya msaada kufanikisha majadiliano yenye tija, akiongeza kuwa vita “haina washindwaji” na kwamba dunia nzima kwa sasa inasubiri kumalizwa kwa vita hivyo.

Zelenskyy aushukia mkutano wa Riyadh, avunja ziara yake ya Saudi Arabia

Zelenskyy alioneshwa kutokufurahishwa kwake na mkutano wa Jumanne kati ya Urusi na Marekani uliofanyika Riyadh, akiweka wazi kuwa Ukraine haikutaarifiwa mapema kuhusu mkutano huo.

"Tulishangazwa sana," alisema, na kuongeza kuwa, mkutano huo usingeezaa matunda yoyote bila uwepo wa Ukraine.

Hali kadhalika, alivunja safari yake ya Saudi Arabia baada ya hatua hiyo, na kwa sasa anasubiria ujumbe wa Marekani jijini Kiev.

Uturuki kama msuluhishi

Erdogan aligusia uwezekano wa Uturuki kuwa mwenyeji wa mazungumzo yajayo ya amani, akisema kuwa jitihada za kidiplomasia za Ankara zinaendelezwa kupitia vikao vya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na majadiliano yake binafsi na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

"Ni matumaini yangu kuwa vikao vyetu vitawezesha upatikanaji wa amani," alisema Erdogan.

Akisisitizia haja ya diplomasia shirikishi, aliongeza, "Uwezo wa kujitawala wa Ukraine ni jambo lisilopingika na Uturuki itaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha kuwa pande zote zinahusishwa."

Vita hivyo vinaendelea huku viongozi hao wakitaka uhuhishwaji wa kidiplomasia.

TRT Afrika