"Mwanadamu anakopa kilio wakati huu. Wale wanaosimama upande sahihi wa historia wanazungumza," Rais Recep Tayyip Erdogan alisema kuhusu ukatili wa Israel huko Gaza, katika safari yake ya kurudi kutoka ziara ya kidiplomasia nchini Algeria.
Katika taarifa zake wakati wa safari hiyo siku ya Jumanne, Rais alilaani ukamataji wa ardhi wa Israel hatua kwa hatua, akilinganisha na wizi, na kuongezea umuhimu wa mabadiliko ya msimamo wa dunia dhidi ya Israel.
"Zama zimebadilika. Unaweza kuona jinsi dunia inavyoanza kuchukua msimamo dhidi ya Israeli. Uvamizi huko Gaza, wakati baadhi ya serikali zinabaki kimya, kwa bahati nzuri umegusa dhamiri za watu. Idadi ya wale wanaounga mkono Palestina mitaani inaongezeka," alisema.
Akitoa mfano wa maandamano ya hivi karibuni mjini Berlin, Uingereza, Marekani, na nchi nyingine, alitaja ongezeko la harakati hata ndani ya Israel, ambapo watu wanataka Waziri Mkuu Netanyahu ajiuzulu.
"Netanyahu yupo katika hali ngumu kisheria. Haijalishi ataenda wapi, hawezi kuepuka. Kwa matumaini, atakusanya vitu vyake na kuondoka hivi karibuni," Erdogan alisema.
Aliendelea kutoa wito wa jitihada za pamoja kimataifa dhidi ya ukandamizaji huko Gaza, akisisitiza umuhimu wa serikali kuzingatia sheria za kimataifa, haki za binadamu, na maadili.
Kuhusu Kituo cha Mpaka cha Rafah
Akielekeza umakini wake kwa hatua chanya kwenye Kituo cha Mpaka cha Rafah Gaza na Misri, Erdogan aliipongeza serikali ya Misri kwa juhudi zake. Alisisitiza idadi inayoongezeka ya wagonjwa wa Gaza wanaopokea matibabu katika hospitali za miji ya Kituruki na kueleza hamu yake ya kurahisisha zaidi uhamishaji wa wagonjwa.
"Tunataka kuwapeleka wagonjwa wote haraka iwezekanavyo. Nataka kuwachukua wale wanaohitaji upasuaji haraka iwezekanavyo, haswa watoto, na kufanya hatua za matibabu."
Akizungumzia vizuizi huko Gaza, Erdogan alisisitiza umuhimu wa mkakati kamili, kushirikisha wanachama wote wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Kiarabu. Aliitaka kutumia vipengele vya kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia, kijamii, na kitamaduni kuanzisha kusitisha mapigano, kutoa misaada kwa Gaza, na kuijenga upya mji.
Kuvunja 'kizuizi cha kiakili'
Rais kwa mara nyingine tena alisisitiza ni lazima kuondoa vizuizi vilivyowekwa na Wazayuni na wafuasi wao, na kuiruhusu Palestina kurudisha mipaka yake ya kihistoria na haki ya kujitawala.
Amesisitiza kuwa ni kupitia juhudi hizo pekee ndipo amani ya kudumu inaweza kupatikana katika eneo hilo.
"Vizuizi sio tu kuhusu wanajeshi na silaha ambazo Israeli imekusanyika karibu na Gaza. Ni lazima tulazimishe Israeli kuzingatia sheria za kimataifa na kuwajibika kwa matendo yake. Kwa mfano, lazima tuvunje kizuizi kwenye jukwaa la Umoja wa Mataifa.
Akilaani mtazamo wa kibaguzi unaodhalilisha maisha ya Waislamu na kutilia mkazo uelewa wa walimwengu kwamba upotevu wowote wa maisha ya mwanadamu ni sababu ya kutia wasiwasi, Erdogan aliendelea kwa kusema, "Lazima tuondoe vizuizi vyote vinavyopofusha lugha na macho ya ulimwengu - vile vilivyowekwa na Wazayuni na wafuasi wao ambao wameinyima Palestina mipaka yake ya kihistoria, haki ya kujitawala kwa watu wake, haki ya mali, haki ya kuishi, na uhuru mwingine. Ni hapo tu ndipo tunaweza kupata amani ya kudumu."
Kuhusu mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas, Erdogan alisema haamini kwamba "Hamas ina au itakuwa na tabia mbaya kwa raia walio chini ya ulinzi wake", akisisitiza kwamba Israel inashikilia idadi kubwa ya Wapalestina, na Hamas inafanya juhudi za kuwaachilia walio nao”
"Kama unavyojua, ushiriki wa Qatar unatoa sura mpya katika mchakato wa amani. Nadhani kubadilishana kwa mateka kutatokea hivi karibuni, "aliongeza.
Uhalifu wa Israeli dhidi ya ubinadamu
Erdogan alisisitiza kuwa, karibia nchi zote za Ulaya ziko kimya kuhusu suala hilo, na hakuna uingiliaji kati wao kuzuia mauaji ya Israeli.
"Ulimwengu wa Kiislamu haupaswi kukaa kimya juu ya uchokozi huu. Kuanguka kwa Gaza kunaweza kumaanisha jeraha kubwa kwa umoja na mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu," alisema.
"Wanasiasa ambao huziba sikio kwa sauti hiyo, hivi karibuni watakabiliwa na matokeo, katika majibu ya kidemokrasia ya watu wao.
Kwa macho ya watu, viongozi ambao, kwa msimamo wao wa kuunga mkono Israel, wanakuwa wafuasi wa mauaji ya halaiki, wanapaswa kurekebisha kosa hili haraka iwezekanavyo,” alisema, akiongeza kuwa serikali zinazoiunga mkono Israel lazima ziepuke kushiriki katika uhalifu huu.
Rais alikariri kwamba mtu hapaswi kukaa kimya na kutojibu uhalifu unaofanywa na Israeli. "Ugaidi wa serikali na wavamizi wa Israel huko Gaza na miji mingine ya Palestina ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, na mauaji ya halaiki," Erdogan alisema.
"Tunashikilia matumaini kuwa matokeo chanya yanakuja kutokea. Ninaamini kuwa uchungu tunaoupata hivi sasa ni sawa na uchungu wa kuzaliwa kwa amani iliyotarajiwa kwa muda mrefu katika eneo letu, na kuanzishwa taifa la Palestina ," aliongeza.
Maendeleo katika tasnia ya ulinzi
Rais wa Uturuki, katika taarifa zake siku ya Jumanne, pia aliangazia maendeleo ya tasnia ya ulinzi asilia, akisisitiza kwamba kila hatua inayochukuliwa na Uturuki katika sekta hii inaijaza nchi msisimko.
"Wale wanaojitolea kwa tasnia ya ulinzi wanatoa mchango mkubwa kwa mustakabali wa nchi yetu na utambuzi wa Karne ya Uturuki," alisema.
"Kaan, Kizilelma, TCG Anadolu na zingine, hazitasimama peke yao. Tunatumai, miradi mipya, iliyoboreshwa na iliyo na vifaa bora itaibuka kupitia juhudi za kujitolea za kaka na dada zetu katika huduma ya nchi yetu."
Alikumbuka kuwa si muda mrefu uliopita, ndege ya anga yasiyo na rubani na risasi za kisasa hazikuwepo katika uwezo wa kijeshi wa Uturuki, lakini nchi hiyo sasa inaweza kufanya maendeleo makubwa katika sekta ya ulinzi.
"Tunajitahidi kupata ubora na wahandisi bora, watengenezaji programu, mafundi na wabunifu."
"Maendeleo mapya yanaendelea, na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Katika sekta ya ulinzi na katika nyanja nyinginezo, tuko tayari kujijengea sifa kubwa zaidi," Rais aliongeza.