Erdogan alisisitiza katika barua hiyo kwamba Uturuki imekuwa nchi ya pili kwa ukubwa kutoa misaada kwa Gaza, ikiwa na karibu tani 45,000 za misaada ya kibinadamu tangu Oktoba 7, 2023. / Picha: AA Archive

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito kwa watu duniani kote kuzungumza juu ya mashambulizi ya Israel dhidi ya hospitali, shule, misikiti na makanisa katika Gaza ya Palestina.

"Ubinadamu lazima uzuie ukiukwaji zaidi wa sheria za kimataifa huko Gaza," Erdogan alisema katika barua kwa Papa Francis siku ya Jumamosi, akisisitiza kwamba watu wasio na hatia na miundombinu ya kiraia haipaswi kulengwa, hata wakati wa vita.

Akisisitiza kwamba mauaji ni marufuku katika imani zote za Ibrahimu, alisema ubinadamu "lazima upaze sauti yake dhidi ya ulipuaji wa makusudi wa hospitali, shule, misikiti na makanisa ambayo hayapaswi kukiukwa, hata wakati wa vita."

"Changamoto zinazotukabili, hususan mashambulizi ya kiholela ya Israel huko Gaza, ambapo vifo vya njaa hutokea kutokana na kushindwa kutoa misaada ya kibinadamu hata wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, na athari za kimataifa za Vita vya Ukraine, ambavyo sasa viko katika mwaka wa tatu, unahitaji jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kwa ushirikiano na uratibu," Erdogan alisema.

Rais wa Uturuki ameongeza kuwa, kupatikana amani na utulivu wa kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati haiwezekani bila ya kuwepo utatuzi wa haki wa suala la Palestina na Israel.

"Nchi huru na iliyounganishwa kijiografia ya Palestina ndani ya mipaka ya 1967, na Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake, lazima ijitokeze na kuchukua nafasi yake katika mfumo wa kimataifa kama mwanachama sawa wa jumuiya ya kimataifa," alisisitiza.

Papa alishukuru kwa juhudi za amani za Erdogan

Mkuu wa Kurugenzi ya Masuala ya Kidini ya Uturuki, Ali Erbas, aliwasilisha barua ya Erdogan wakati wa ziara yake kwa Papa, ambaye alisema alimshukuru rais kwa "alichofanya."

"Papa Francis alisisitiza kwamba rais wetu ni mmoja wa viongozi wachache wanaofanya kazi kwa bidii kwa ajili ya amani ya dunia, na ambaye ana uwezo wa kufanikisha hili," Erbas alisema.

Erbas pia alisema lengo la mkutano wao lilikuwa "mauaji, na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa na Israeli huko Palestina."

"Yerusalemu, kielelezo cha amani na kuishi pamoja, iko chini ya ukandamizaji wa Israeli, kila mahali, bila kujali Waislamu au Wakristo, watoto wachanga au watoto wasio na hatia, misikiti au makanisa. Tunakabiliwa na hali ambapo kila mtu, ikiwa ni pamoja na watoto, wazee, wagonjwa na wanawake; wanauawa kwa umati," Erbas aliongeza.

"Tulielezea haja ya kufanya kazi kwa pamoja ili kukomesha hali hii na kutoa tahadhari zaidi kwa Palestina na Gaza na kukomesha ukandamizaji wa Israel."

Vita vya Israel dhidi ya Wapalestina waliozingirwa wa Gaza - sasa katika siku yake ya 190 - vimewauwa Wapalestina wasiopungua 33,686 na kujeruhi wengine zaidi ya 76,309 tangu shambulio la kuvuka mpaka la kundi la Hamas la Palestina Oktoba 7, ambalo liliua takriban watu 1,200.

Israel inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Uamuzi wa muda wa mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv kusitisha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba msaada wa kibinadamu unatolewa kwa raia huko Gaza.

TRT World