Waziri huyo aliitaka jumuiya ya kimataifa kutumia kila aina ya shinikizo la kimataifa kumaliza mgogoro huo. / Picha: AA  

Israeli imepeleka "ukatili wa kimfumo" katika eneo la Gaza ya Palestina, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amesema.

"Israeli sio tu inafanya mauaji ya halaiki huko Gaza, lakini sasa inaendeleza vita hivi hadi Ukingo wa Magharibi, Lebanon, na uwezekano wa mataifa mengine ambayo inaona kama maadui ambao hatuwezi kujua au kutabiri," Fidan alisema katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake kutoka Slovenia, katika eneo la Ljubljana siku ya Ijumaa.

Fidan amesema Israeli imekuwa ikifanya uvamizi, ukandamizaji, ukatili na mauaji ya halaiki katika eneo hilo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kukomesha jinai zinazofanywa na Israeli katika ardhi za Palestina.

Toka Oktoba 7, mauaji ya kimbari yamekuwa yakitokea Gaza, na Israeli ikiwaacha watu wa Gaza katika njaa na kiu.

Israeli imekanyaga tunu zote za kibinadamu kwa kulipua hospitali, misikiti, shule na makanisa kwa mabomu, aliongeza.

"Serikali ya Netanyahu inaendelea kucheza na moto. Inahatarisha mustakabali wa eneo zima kudumisha msimamo wake. Kila anayekaa kimya juu ya suala la Gaza, haswa wale wanaoiunga mkono Israeli bila masharti, yuko chini ya mzigo. Ushenzi wa Israeli lazima uhitimishwe ,” aliongeza.

Njia pekee ya kufikia amani ya kudumu

Waziri huyo pia alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutumia mbinu zote zilizopo za shinikizo la kidiplomasia ili kukomesha mzozo huo. Alisisitiza kwamba wakati baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Uturuki, zimechukua misimamo dhabiti ya kiuchumi, kibiashara na kisiasa, utaratibu mpana na wenye ufanisi zaidi wa shinikizo ni muhimu.

"Kama vile tunavyopinga uvamizi wa ardhi ya Ukraine, pia tunapinga uvamizi wa maeneo ya Palestina na Israeli," alisema, akiitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti.

Alisisitizia msimamo wa muda mrefu wa Uturuki wa kaunzishwa kwa taifa huru la Palestina ndani ya mipaka ya 1967, na Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake, kama suluhisho pekee la mgogoro huo.

"Tutaendelea na juhudi zetu ili kufanikisha hili bila kuchoka," aliongeza.

Fidan pia aliipongeza Slovenia kwa kuwa kuliongoza baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huku akisifia msimamo thabiti wa nchi hiyo katika kuitambua Palestina kama dola.

"Ni imani yangu kuwa tunaweza kuongeza jitihada zetu za pamoja ili kupata suluhisho la haki na la kudumu la Palestina," alisema Fidan.

Uhusiano na Slovenia

Katika kuimarisha uhusiano na Slovenia, Fidan alisema: “ Kama ishara ya nia hii, tumeandaa na kutia saini mpango mkakati wa kipindi cha 2024-2026. Njia hii itatusaidia kuendeleza mahusiano yetu katika kila nyanja na hatua.”

Akisifia kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili, Fidan alieleza kuridhishwa na ushiriki wa makampuni ya Uturuki katika miradi nchini Slovenia.

Fidan alisema usafiri una jukumu muhimu katika biashara kwa hivyo Uturuki inapendelea ukombozi kamili katika hati za usafirishaji wa nchi kavu.

Ukombozi kamili ungechangia katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Ulaya na Asia, aliongeza.

Israeli imeendeleza mashambulizi yake ya kikatili huko Gaza tangu Oktoba 7, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano.

Mauaji hayo yamepelekea vifo vya zaidi ya Wapalestina 40,600, wengi wakiwa ni wanawake na watoto na majeruhi wengine zaidi ya 93,800, kulingana na duru za afya.

Vikwazo vinavyoendelea Gaza vimesababisha uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, na kuacha sehemu kubwa ya eneo hilo kuwa magofu.

Israeli inakabiliwa na tuhuma za mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ambayo imeamuru kusitishwa kwa mashambulizi ya kikatili katika mji wa kusini wa Rafah, ambapo zaidi ya Wapalestina milioni moja walikuwa wametafuta hifadhi kabla ya eneo hilo kuvamiwa Mei 6.