Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa wito kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuitisha mkutano wa dharura wa ngazi ya uongozi ili kukabiliana na mashambulizi yanayoongezeka dhidi ya Jerusalem.
Rais Erdogan alisema serikali ya Israeli inataka kupanua sera zake za uvamizi na kukalia kwa mabavu ili kujumuisha Msikiti wa Al Aqsa, ambao ni muhimu kwa Waislamu kama Kibla chao cha kwanza.
"Ni jambo lisilowazika kwamba Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, ambayo wajibu wake ni kutetea kadhia ya Al Quds, ingebaki kutojali mashambulizi haya ya kiholela amabayo yanazidi siku baada ya siku," Erdogan alisema baada ya mkutano na baraza la mawaziri siku ya Jumatatu.
Erdogan alisisitiza ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka na kusisitiza ya kwamba: " Ni dharura kwa Jumuia ya (OIC) ikutane katika ngazi ya uongozi bila kuchelewa na kwamba ulimwengu wa Kiislamu uonyeshe misimamo yake thabiti."
"Tutachukua kila hatua ya kisheria"
Kuhusu kifo cha Aysenur Ezgi Eygi, mwanaharakati wa Uturuki na Marekani aliyeuawa na majeshi ya Israeli, Rais Erdogan aliapa kutafuta haki.
"Tutachukua kila hatua ya kisheria ili kuhakikisha kuwa damu ya Aysenur Ezgi haiachiwi bila kulipizwa kisasi, na tutaendeleza mapambano yetu dhidi ya Israeli kwa kiwango cha juu zaidi kwa kutuma ombi kwa Mahakama ya Haki," alisema.
Eygi aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israeli siku ya Ijumaa wakati wa maandamano dhidi ya makazi haramu ya Waisraeli katika mji wa Beita katika wilaya ya Nablus katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Pia alionyesha mshikamano na watu wa Palestina, akisema, "Kama taifa ambalo liliweka historia ya kishujaa ya ukaidi dhidi ya madola ya kibeberu wakati wa Vita vya Uhuru, tunasimama na ndugu zetu wa Palestina."