Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesisitiza wito wake wa kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia kura ya turufu ya Marekani ya azimio lililotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano ya kibinadamu huko Gaza siku moja kabla.
"Kutokana na kura ya turufu ya Marekani, hakuna uamuzi uliofikiwa. Ni muhimu kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanyiwa mageuzi," Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema katika hotuba yake Jumamosi kwenye hafla ya Siku ya Haki za Kibinadamu Duniani huko Istanbul.
"Tumepoteza matumaini na matarajio yetu kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," alisema.
"Tangu Oktoba 7, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo dhamira yake ni kuleta amani duniani, limegeuka kuwa mlinzi wa Israel."
Israel ilianza tena mashambulizi yake ya kijeshi huko Gaza tarehe 1 Disemba baada ya kumalizika kwa mapatano ya wiki moja na kundi la muqawama la Palestina Hamas.
Takriban Wapalestina 17,500 wameuawa katika eneo lililozingirwa katika mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel tangu mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba.
'Wachinjaji wa Gaza wawajibishwe'
Erdogan alisisitiza kuwa, serikali ya Israel, ikiungwa mkono na kamili na nchi za Magharibi, inafanya ukatili na mauaji makubwa huko Gaza ambayo yanaaibisha ubinadamu kwa ujumla.
"Wachinjaji wa Gaza" lazima wawajibike kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, Erdogan alisema, akiongeza kuwa watawajibishwa "mapema au baadaye."
Alisema ulimwengu wa haki unawezekana, lakini si kwa Marekani kwa sababu inaungana na Israel.
Rais wa Uturuki alisema Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Kibinadamu linakiukwa vikali huko Gaza, na maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.