Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikutana na viongozi wa Ethiopia na Somalia kupatanisha nchi hizo mbili mwezi uliopita. /Picha: AA

Na Ahmet Yusuf Ozdemir

Mwezi uliopita, Ankara iliandaa mkutano wa kihistoria kati ya nchi mbili zilizoko kwenye eneo la kimkakati katika Pembe ya Afrika: Ethiopia na Somalia. Nchi zote mbili zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia lakini wenye mgogoro kwa karibu miongo mitatu.

"Upatanisho wa kihistoria" unaosimamiwa na Uturuki wa kati ya Somalia na Ethiopia unawakilisha maendeleo makubwa katika usimamizi wa migogoro, kuweka diplomasia ya Ankara na sera ya kigeni tofauti na mataifa yenye nguvu na ushawishi kama vile Marekani, China na Umoja wa Ulaya.

Hapo awali, eneo la Pembe ya Afrika kwa ujumla na hasa mzozo wa Somalia, ulisababisha nchi kuwekeza katika misaada ya kibinadamu au kijeshi ili kudhoofisha Al Shabab. Ilionekana kuwa mzozo huu haungeweza kutatuliwa bila kuzingatia nchi jirani ya Ethiopia.

Hii sasa ndio inaifanya nafasi ya Uturuki kuwa ya kipekee. Ilifanya kazi kwa msingi kwamba maadamu uadui kati ya nchi hizo mbili za Kiafrika ungekuwepo, hakutakuwa na suluhu zozote thabiti na za kudumu kwa mgogoro huo.

Kulingana na ripoti kutoka Chuo cha Geneva, Afrika inashika nafasi ya pili baada ya Mashariki ya Kati katika masuala ya migogoro ya kivita kwa kila eneo. Kwa sasa bara hilo linakabiliwa na migogoro zaidi ya 35 ya silaha zisizo za kimataifa, ikiwemo Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Mali, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Somalia, Sudan Kusini na Sudan.

Makundi mengi yenye silaha yanahusika katika migogoro hii, ama yanapingana na majeshi ya serikali au yanapigana wenyewe kwa wenyewe. Mataifa yenye nguvu ya Magharibi na mataifa jirani yameingilia kati migogoro ya silaha isiyo ya kimataifa inayotokea Burkina Faso, Mali, Msumbiji, Nigeria na Somalia.

Ikilinganishwa na vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe ulimwenguni kote, kama vile Colombia, Ufilipino, au Afghanistan, mizozo barani Afrika ni nadra sana kusuluhishwa kupitia mazungumzo ya amani na suluhu. Hili linaweza kubadilika kwani Somalia na Ethiopia hatimaye zimekubali kusuluhisha tofauti zao.

Chini ya Azimio la Ankara, mataifa hayo mawili yataanza mazungumzo kabla ya Februari, kwa uwezeshaji wa Uturuki, na kuhitimishwa na kutiwa saini katika miezi minne.

"Mkataba kati ya majirani wawili (Somalia na Ethiopia) sasa umetuliza hofu ya mzozo mpana wa kikanda katika Pembe ya Afrika," kulingana na Emmanuel Onyango na Tuğrul Oğuzhan Yılmaz katika makala ya TRT Afrika.

"Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Pembe ya Afrika (IGAD), ilikaribisha mkataba huo na kuipongeza Uturuki kwa juhudi zake za upatanishi."

Changamoto za Somalia

Nchini Somalia, Al Shabab ina chukua nafasi muhimu katika kuifanya Pembe ya Afrika kuwa moja ya maeneo yenye migogoro. Zaidi ya hayo, uwepo wa jumbe za kimataifa zaidi ya moja nchini humo, hasa Ujumbe wa AUSSOM na UNTMIS, unafanya mzozo huo, kwa namna fulani, kulinganishwa na mfano wa uhusiano kati ya Marekani na Taliban.

Kikundi cha kigaidi cha Al Shabab kinachukuliwa kuwa na nafasi muhimu katika kukosekana kwa utulivu katika Pembe ya Afrika. /Picha: AP

Somalia inasalia kuwa moja ya vituo muhimu zaidi vya mfumo wa kimataifa wa baada ya Vita Baridi. Ilikuwa ni moja ya nchi za kwanza zilizoshuhudia mazungumzo ya uingiliaji wa kibinadamu ambayo yaliibuka na kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.

Mnamo 1991, mchakato ulioanza kwa kuanguka kwa utawala wa Siad Barre baada ya kushika madaraka tangu 1969, uliiingiza nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Vita hivi kati ya makabila na wababe wa vita vilikabiliwa na hatua za kikanda na za kimataifa.

Hasa, juhudi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na oparesheni za "misaada ya kibinadamu" za Jeshi la Marekani zilisababisha mzozo mwaka 1992. Hata hivyo, uingiliaji kati huu uliunda seti yake ya matatizo.

Ni muhimu kukumbuka kutofaulu kwa muda mrefu kwa jumuiya ya kimataifa katika kusaidia taifa hilo kujijenga upya. Kwa mfano Afghanistan, baada ya uvamizi wa Umoja wa Kisovyeti, Marekani iliunga mkono upinzani wa Afghanistan kuwashinda wavamizi. Lakini wakati Wasovieti walipojiondoa kutoka Afghanistan, na Marekani pia walijiondoa.

Uundaji upya wa baada ya vita, mabadiliko, na taratibu za haki za mpito, ikimaanisha jinsi jamii zinavyoitikia ukiukaji mkubwa na mbaya wa haki za binadamu, hazikuanzishwa nchini Somalia wala Afghanistan.

Kujaza pengo

Kutokua na serikali baada ya Umoja wa Mataifa na Marekani kujiondoa kutoka Somalia katika miaka ya 90 lilijazwa na watendaji wa kikanda. Nchi jirani ya Somalia, Ethiopia ilichukua nafasi muhimu baada ya 1996 kwa kuanzisha uvamizi wa kuvuka mpaka.

Mnamo mwaka wa 2005, Muungano wa Mahakama za Kiislamu, ambao ulikuwa umejitengenezea nyanja ya ushawishi, uliwashinda wababe wa kivita mwaka 2006 na kutangaza mamlaka yake nchini Somalia, jambo ambalo lilisababisha uingiliaji mpya wa Ethiopia nchini humo.

Ethiopia, ikiungwa mkono kisiasa na Marekani na kijeshi na Uganda, pamoja na Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na Serikali ya Mpito ya Shirikisho, ilidumisha utawala wake hadi 2009.

Mwaka huo huo, Al Shabab walichukua fursa ya kutokua na serikali iliotokana na kujiondoa kwa Ethiopia nchini humo na kuweka mfumo wake wa utawala, na kudumisha udhibiti wa eneo la kusini mwa nchi hiyo.

Tangu kuanzishwa kwake na haswa baada ya kuunga mkono kundi la Al Qaeda mnamo 2012, Al Shabab ikawa shabaha nambari moja ya Marekani ya 'Vita dhidi ya Ugaidi' katika eneo hilo.

Baada ya miaka 18 ya ukatili mkubwa ndani ya Somalia, pamoja na nchi jirani za Kenya na Ethiopia, Al Shabab ilishuhudia kushindwa kijeshi, kurudi nyuma pamoja na kujipanga upya.

Stig Jarle Hansen, mmoja wa wataalam wakuu wa Al Shabab, anahoji kwamba ulipaji kodi haramu, mashindano ya jumuiya, udhaifu wa jeshi, na kuwepo kwa maeneo salama vimekuwa baadhi ya vipengele muhimu vya kuendelea kwa Al Shabab.

Mangamuzi ya ndani, kikanda na kimataifa unaweza kusaidia utekelezaji wa sheria kukomesha ongezeko la Al Shabab katika Pembe ya Afrika.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Utawala wa Taasisi za Sheria na Usalama, iliyoanzishwa ndani ya Idara ya Operesheni za Amani, ina sehemu chini ya mamlaka yake inayoitwa upokonyaji silaha.

Lengo kuu la mchakato huu ni kuchangia usalama na utulivu katika mazingira ya baada ya migogoro ili ahueni na maendeleo yaanze. Hii ilitumika kwa migogoro ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Burundi, Colombia, Ethiopia, Haiti, Iraq, Libya, Yemen na Somalia.

Kiongozi wa zamani wa Al Shabab, Mukhtar Robow, alipata kuwa Waziri wa Masuala ya Kidini wa Somalia baada ya kuondoka kwenye kundi hilo. /Picha: Reuters.

Moja ya mifano maarufu zaidi ya hii ni Mukhtar Robow, naibu kiongozi wa zamani na msemaji wa Al Shabab, ambaye aliondoka kwenye kundi hilo mnamo 2015 na kuteuliwa kuwa Waziri wa Masuala ya Kidini wa Somalia. Mifano kama hii inahitaji kupanuliwa ili kusisitiza ukweli kwamba njia ya Al Shabab ya kutoa changamoto kwa serikali na kuvuruga amani katika eneo hilo haiwezi kuendelea.

Azimio la Ankara

Azimio la Ankara ambalo lilitangazwa kati ya Somalia na Ethiopia linaweka msingi wa mazungumzo sawa ya siku zijazo ili kupigana na Al Shabab kwani nchi zote mbili ni walengwa na wahanga wa harakati hii na wana uzoefu mkubwa katika eneo hilo.

Taarifa rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Uturuki ilitangaza "Walikubaliana, kwa moyo wa urafiki na kuheshimiana, kuacha tofauti na masuala yenye utata na kusonga mbele kwa njia ya ushirikiano ili kutafuta ustawi wa pamoja."

Amani yenye nguvu na ya kudumu inaweza tu kutokea kwa mtazamo kamili badala ya nchi moja kuhangaika yenyewe. Uzoefu, akili, na kushiriki ujuzi ni muhimu kwa mzozo wowote kufikia kikomo.

Hili lilikuwa mojawapo ya kushindwa kwa kiutendaji katika mazungumzo kati ya Marekani na Taliban nchini Afghanistan.

Ingawa Marekani haikuwa ikifanya kazi kivyake nchini Afghanistan lakini ikiwa na muungano wa kimataifa tangu 2001, haikushirikisha pande nyingine kwa ajili ya amani endelevu ambayo ingemnufaisha kila mtu katika eneo hilo.

Ikilinganishwa na mtazamo wa Marekani, mpango wa Uturuki wa kumaliza mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa kwa kuruhusu pande zinazohusika kuketi kwenye meza moja kujadili changamoto zilizopo ni jambo ambalo eneo la Pembe ya Afrika limekuwa likisubiri.

Mwandishi, Ahmet Yusuf Ozdemir, ni Profesa Msaidizi wa Sayansi ya Siasa na Idara ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Ibn Haldun.

Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.

TRT Afrika