Mabingwa wa ligi mbalimbali ya kina dada wameanza safari ya kuelekea Kampala Uganda kwenye ngarambe za mechi za kufuzu za kumsaka mwakilishi wa Afrika Mashariki ukanda wa CECAFA kwenye fainali za kombe la CAF.
Kulingana na ratiba ya mechi hizo, Kampala Queens ya Uganda itaungana na CBE ya Ethiopia iliyotua fainali ya makala yaliyopita.FAD ya Djibouti, Buja Queens ya Burundi pamoja na Yei Joints ya Sudan wamekutana kwenye Kundi A, huku Kundi B, ikijumuisha JKT Queens ya Tanzania, Vihiga Queens ya Kenya, AS Kigali ya Rwanda na New Generation ya Zanzibar.
Droo ya mechi hizo za Kufuzu kwa makala ya tatu ya Ligi ya Mabingwa wa CAF ya Wanawake, Cote D'Ivoire 2023, ilifanyika rasmi Julai mwezi uliopita kwenye Uwanja wa Mohammed VI huko Rabat, Morocco.
Tayari wawakilishi wa Tanzania Jkt Queens wakiongozwa na benchi la ufundi na Viongozi, wamewasili Bukoba mkoani Kagera kuweka kambi ya mazoezi ya mwisho siku chache kabla ya kushuka dimbani.
Mabingwa mara nne wa ligi kuu ya wanawake Kenya, Vihiga Queens ambao pia waliwahi kuiwakilisha ukanda wa Cecafa, nao wameendelea na mazoezi yao huku wakimsajili kocha mkuu mpya Charles Okere kuongoza maandalizi ya klabu hiyo.
Hata hivyo, wawakilishi wa Sudan Kusini kwenye mashindano hayo, Yei Joint Stars imeeleza kukabiliwa na changamoto za kifedha huku klabu hiyo ikiitisha msaada kujiandaa vilivyo kwa makala hayo.
Licha ya kueleza kuwa itaeleekea Uganda siku ya jumatano, mabingwa hao wa mara tatu wa ligi kuu ya soka ya wanawake Sudan Kusini, wamewaomba wasamaria wema kuichangia kifedha ili kuiwezesha kujiandaa vikamilifu.