Victor Osimhen alitajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika mapema mwezi huu, Disemba. Picha: CAF

Mkataba wa awali wa Osimhen ungemalizika Juni 2025 na urefushaji wake umekuwa gumzo nchini Italia tangu Napoli ilipotwaa taji lao la kwanza la ligi baada ya zaidi ya miongo mitatu msimu uliopita, chini ya kocha wa zamani Luciano Spalletti.

Napoli ilitangaza taarifa hiyo iliyosubiriwa kwa muda mrefu na ujumbe mfupi katika mitandao ya kijamii "Victor na Napoli pamoja hadi 2026," pamoja na picha za mshambuliaji Wa Nigeria akiweka kalamu kwenye karatasi pamoja na mmiliki wa kilabu Aurelio De Laurentiis.

Klabu hiyo ya Napoli hata hivyo haijafichua maelezo zaidi kuhusu mkataba huo, lakini vyombo vya habari vya Italia vinaripoti kwamba Osimhen amewekewa kitita cha uhamisho kuondoka timu hiyo chenye thamani ya Euro milioni 130 (dola million 143) ili kuhakikisha klabu hiyo haipotezi mchezaji wao nyota virahisi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 pia anaripotiwa kuwa atakuwa akipokea Euro milioni 10 kila mwaka baada ya kutozwa kodi.

Osimhen aliifunga Napoli mabao 26 ya ligi Napoli iliyovutia Ulaya kwa mchezo wake wenye kusisimua na kutawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza tangu Diego Maradona alipokuwa akiichezea klabu hiyo.

Kwa jumla, Osimhen, mshindi wa tuzo ya mchezaji Bora wa mwaka wa Afrika CAF, ameifungia Napoli mabao 67 ndani ya mechi 118 tangu aliposainiwa kutoka Lille mnamo 2020 kwa Euro milioni 70 za awali.

Staa huyo Osimhen amesaini mkataba huu mpya muda mfupi kabla ya kufunga safari kuelekea Ivory Coast ambapo Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon litaanza kuanzia Januari 13.

TRT Afrika na mashirika ya habari