Manchester City imetwaa taji la nne la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), na kuwa timu ya kwanza kushinda kombe hilo mfululizo.
Kikosi cha Pep Guardiola kiliwafunga West Ham United mabao 3-1 katika mchezo wao wa mwisho katika uwanja wa Etihad na kunyakua taji hilo, huku kukiwa na mchuano mkali kati yake na Arsenal, ambayo imeshika nafasi ya pili.
City wamekamilisha msimu wa 2023/24 wakiwa na pointi 91, mbili mbele ya Arsenal, na bado wako kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kombe la FA katika fainali dhidi ya wapinzani wao Manchester United kwenye Uwanja wa Wembley Jumamosi, Mei 25.
Msururu wa vikombe
Hili linakuwa taji la 10 la Ligi Kuu kwa Manchester City katika historia ya klabu hiyo, na la saba tangu wamiliki wao wa Abu Dhabi City Football Group wachukue timu ya Uingereza mwaka 2008.
Kwa sasa, Guardiola ameshinda mataji 17 ya dhahabu tangu ajiunge na City, mataji ambayo yanajumuisha sita ya Ligi Kuu, moja la Ligi ya Mabingwa, mawili ya Kombe la FA, manne ya Kombe la Ligi, moja la UEFA Super Cup, moja la Kombe la Dunia la Klabu ya FIFA na Ngao mbili za Jamii.
Sita bora Ligi Kuu ya Uingereza:
Manchester City – alama 91
Arsenal – alama 89
Liverpool – alama 82
Aston Villa – alama 68
Tottenham Hotspur – alama 66
Chelsea – alama 63