Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, na mwenzake wa Kuwait, Jarrah Jaber Al Ahmad AlSabah, wamejadili hali ya hivi karibuni katika ukanda huo kupitia mazungumzo ya simu, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya Uturuki.
Mazungumzo hayo yalifanyika baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema mapema kuwa mazungumzo mapya kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kuanza Jumatatu alasiri.
Vyanzo hivyo vya kidiplomasia havikutoa maelezo zaidi kuhusu mazungumzo ya simu yaliyofanyika Jumatatu.
Siku ya Jumamosi, Kuwait ilitangaza kuwa jeshi lake liliharibu ndege zisizo na rubani za Iran baada ya mashambulizi yaliyolenga kituo cha serikali pamoja na magari ya kampuni ya kiraia katika Kisiwa cha Bubiyan. Mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu wa mali lakini hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa au kupoteza maisha.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Kuwait, Saud Al-Atwan, alisema vikosi vya ulinzi viligundua "droni za uhasama" katika anga ya Kuwait tangu mapema Jumamosi na kufanikiwa kuziharibu.
Aliongeza kuwa "uchokozi wa Iran" ulilenga miundombinu kadhaa muhimu, ikiwemo kituo cha serikali kaskazini mwa Kuwait na magari ya kampuni ya kiraia katika Kisiwa cha Bubiyan. Pia alisema mabaki ya droni zilizoangushwa yalisababisha uharibifu wa mali, lakini hakuna majeruhi walioripotiwa.
Mvutano katika ukanda huo umeongezeka tangu Februari, baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya Iran, huku Iran ikijibu kwa kurusha makombora na droni zilizolenga nchi za Ghuba zinazohifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani.
Vyanzo vya serikali ya Pakistan vimeiambia Shirika la Habari la Anadolu siku ya Jumatatu kuwa bado hakuna tarehe wala mahali palipopangwa rasmi kwa ajili ya kuanza tena mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran, ambayo yamekwama kwa muda mrefu. Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi kadhaa kati ya pande hizo mbili.
Mapema Jumatatu, Rais wa Marekani Donald Trump alisema mazungumzo mapya na Iran yataanza alasiri baada ya kuamua kuahirisha mashambulizi dhidi ya Iran. Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, alisema siku hiyo kuwa Tehran haikuwa katika mazungumzo yoyote na Marekani.






















