Muungano wa waasi wa AFC/M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wametangaza kuweka vikwazo vipya vya usafiri vya kuingia na kutoka katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ambako ugonjwa wa Ebola umeenea na kuathiri watu wengi.
Waasi hao wameonesha uwezo wao wa kukabiliana na kuzuia kuenea kwa Ebola.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatano usiku, huduma za usafiri wa teksi za pamoja katika barabara inayounganisha Goma na Kirumba zitasimamishwa kwa mwezi mmoja kuanzia Jumamosi.
Aidha, boti zinazobeba abiria katika baadhi ya njia za Ziwa Edward zitasimamishwa.
Hata hivyo, mabasi madogo ya abiria yataruhusiwa kuendelea na safari katika barabara ya Goma-Kirumba, kwa kuzingatia masharti ya afya na usalama. Malori yanayosafirisha bidhaa pia yataruhusiwa kuendelea na shughuli zake.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wasafiri wawili kutoka mji wa Lubero unaodhibitiwa na serikali kupimwa na kuthibitishwa kuwa na Ebola katika kijiji kilicho chini ya udhibiti wa M23.
Hayo yamesemwa na mmoja wa wajumbe wa timu ya kukabiliana na Ebola iliyoanzishwa na mamlaka za waasi.
Hatua hiyo inaonesha ugumu wa kukabiliana na mlipuko huo wa Ebola, ambao maafisa wa afya wameuelezea kuwa unaenea kwa kasi zaidi kuwahi kurekodiwa, huku mapigano yakiendelea kati ya serikali ya Congo na kundi la waasi linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Waasi wa AFC/M23 wanadhibiti maeneo makubwa ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini baada ya kusonga mbele mwanzoni mwa mwaka 2025, na hivyo kuyateka maeneo ya Goma na Bukavu, miji miwili mikubwa zaidi mashariki mwa Congo.
Umoja wa Mataifa na serikali za nchi za Magharibi zinasema kundi hilo linaungwa mkono na Rwanda, madai ambayo serikali ya Kigali imekanusha.
Waasi hao wametumia mlipuko wa Ebola kuonesha uwezo wao wa kuendesha utawala katika maeneo ya mashariki mwa Congo, kwa kuendesha juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa bila kutegemea mamlaka za serikali kuu zilizoko Kinshasa.
Mwishoni mwa Juni, waasi hao walitangaza kuwa maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao hayakuwa na Ebola.
Kwa mujibu wa takwimu za serikali zilizotolewa wiki hii, idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na Ebola nchini Congo imevuka 5,000.












