| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Mkuu wa mawasiliano wa Uturuki anasema Israel inahujumu juhudi za amani za Gaza
Burhanettin Duran ameeleza dhamira ya Uturuki kusisitiza haki za msingi za watu wa Palestina.
Mkuu wa mawasiliano wa Uturuki anasema Israel inahujumu juhudi za amani za Gaza
Watu wa Palestina wakiwa katika eneo moja baada ya shambulizi la Israel la usiku katika ghala la dawa eneo la Deir al-Balah Agosti 1, 2026. / Reuters

Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki Burhanettin Duran siku ya Jumatatu alishtumu mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yaliyolenga Wapalestina, akieleza kuwa mashambulizi ya Israel "yanahujumu kwa maksudi" juhudi zote za upatikanaji wa amani Gaza.

“Katika kipindi ambacho mipango ya kidiplomasia yenye lengo la kufikia kusitishwa mapigano na kupatikana kwa amani ya kudumu Gaza zinaleta matumaini, mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yanayolenga raia na miundombinu ya afya yanahujumu kwa maksudi juhudi zote za kupatikana kwa amani," Duran alisema katika mtandao wa kijamii wa Uturuki NSosyal.

Duran alieleza kuwa mashambulizi haya, ambayo hayaheshimu haki za maisha ya wanawake, watoto, na raia wasio na hatia, yanaonesha wazi kuwa serikali ya Benjamin Netanyahu haina nia ya kumaliza vita lakini lengo lake ni kuendeleza mzozo tu.

Alitoa wito kwa ulimwengu "kuwa na msimamo thabiti na wa dhati ili kuzuia sera ya uchokozi, ambayo inatishia usalama katika kanda."

"Chini ya uongozi wa Rais wetu Recep Tayyip Erdogan, Uturuki itaendelea kuheshimu sheria ya kimataifa, heshima kwa watu na haki ya msingi ya watu wa Palestina, na kuunga mkono juhudi zote zenye lengo za kupatikana kwa amani ya haki na ya kudumu," aliongeza.

Mashambulizi ya angani ya Israel licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano

Mashambulizi ya angani ya Israel yalilenga Gaza kwa siku ya pili mfululizo siku ya Jumapili, na kuwaua Wapalestina wasiopungua 18, wahudumu wa afya walisema, licha ya tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mafanikio katika juhudi za kutekeleza makubaliano ya mwaka jana ya kusitisha mapigano.

Kuanzia asubuhi, ndege za Israel zilishambulia mashariki mwa Gaza, katikati mwa mji wa Deir al-Balah na eneo la kusini la Khan Younis, kusababisha idadi kubwa ya mauaji kuwahi kutokea katika kipindi cha wiki kadhaa, kulingana na maafisa wa afya wa Palestina.

Mashambulizi ya Deir al-Balah yaliwaua watu wasiopungua wanne, maafisa wa afya wa Palestina walisema, na shambulizi lingine likawajeruhi watu watano na kuchoma moto baadhi ya mahema eneo la Mawasi, karibu na Khan Younis, kulingana na idara ya huduma za dharura.

Familia moja na mtoto wao wa kiume wa miaka 9 waliuawa waliposhambuliwa katika nyumba moja huko eneo la Mawasi, maafisa wa Palestina walisema.

Familia nyingine iliuawa ikiwa pamoja na mtoto wao kutokana na shambulio katika nyumba yao Gaza, ambapo watu wawili zaidi waliuawa kutokana na shambulio kwenye hema karibu na ubalozi wa Misri, wahudumu wa afya walisema. Baadaye siku ya Jumapili, watu wengine wawili waliuawa katika mtaa wa mashariki wa Zeitoun, waliongeza.

Mtu mmoja aliuawa karibu na eneo la Jabalia kaskazini mwa Gaza, maafisa wa Palestina wanasema.

Bodi ya Amani ya Trump, inayoratibiwa na Marekani kufuatilia kusitishwa kwa mapigano, ilichapisha siku ya Ijumaa mpango wa vipengele 15 kueleza hatua za mwisho za utekelezaji wa makubaliano.

Nickolay Mladenov, Mjumbe kiongozi wa Bodi hiyo wa Gaza, anasema mashambulizi kote Gaza yanaendelea licha ya juhudi za bodi na wapatanishi kuleta pande zote za Palestina pamoja ili kukubaliana kuhusu mchakato wa utekelezaji wa mpango wa Trump.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa X alisema wanashirikiana na pande zote, wapatanishi na washirika katika kanda "kusitisha uhasama na kutoa fursa kwa utekelezaji kamili wa mpango wa Rais".

CHANZO:TRT World and Agencies