CAF yatangaza orodha ya wawaniaji wa tuzo za mchezaji bora Afrika 2023

Shirikisho la Soka barani CAF limetangaza orodha ya wanasoka watakaowania tuzo ya mchezaji bora Afrika 2023.

Kulingana na orodha hiyo, nyota wa Afrika wanaozidi kung'aa kwenye mpira duniani wakiwemo Victor Osimhen, Riyad Mahrez, Hakim Ziyech, Mohamed Salah wanawania tuzo hiyo pia.

Orodha hiyo ya wachezaji 30 iliyowajumuisha mastaa wanaosakata soka ya kulipwa barani na nje ya bara, katika ligi mbalimbali, imezinduliwa leo huku ikiwa na majina tajika.

Kwa mujibu wa CAF, kwa mara ya kwanza, CAF imezindua kitengo cha kipa bora wa Afrika CAF kwa Wanaume na Wanawake.

Vitengo vingine ni pamoja na kitengo cha timu bora ya Taifa ya CAF, ambapo Tanzania itamenyana na Cape Verde, Gambia, Guinea Bissau, Equatorial Guinea, Mauritania, Morocco, Msumbiji, Namibia na Senegal.

ACHRAF HAKIMI PSG

Timu ya taifa ya Morocco imekuwa na wachezaji mbalimbali wakiwemo Achraf Hakimi anayepiga huko Paris Saint-Germain, Sofyan Amrabat wa Manchester United, Hakim Ziyech wa klabu ya Uturuki ya Galatasaray, Yassine Bounou wa Al Hilal, Azzedine Ounahi wa Olympique Marseille, Yahya Jabrane wa Wydad Athletic Club, na Youssef En-Nesyri wa klabu ya Sevilla ya Uhispania.

Aidha, Ghana imewakilishwa na Thomas Partey wa Arsenal, na Mohammed Kudus wa West Ham.

Sadio Mane anayecheza Al Nassr ya Saudi, amewaongoza wachezaji wa Senegal kwenye orodha hiyo akiwemo Pape Matar Sarr wa Tottenham Hotspur.

Algeria inawakilishwa na Ramy Bensebaini wa Borussia Dortmund, na Riyad Mahrez wa Al Ahli.

Mohamed Salah wa Liverpool ameongoza wachezaji wa Misri kwenye orodha hiyo wakiwemo Mahmoud Abdel Moneim “Kahraba”, Mohamed Abdelmonem, na Mohamed ElShenawy wanaocheza klabu ya Al Ahly. Aidha nyota wa Afrika Kusini na Al Ahly Percy Tau pia maejumuishwa kwenye orodha hiyo.

Wachezaji Mane, Salah na Onana

Wengine ni Victor Osimhen wa Nigeria na SSC Napoli, Edmond Tapsoba wa Burkina Faso na Bayer Leverkusen, Andre-Frank Zambo Anguissa wa Kamerun na SSC Napoli, Vincent Aboubacar wa Cameroon na Besiktas, Ibrahima Sangare wa Cote d’Ivoire na Nottingham Forest, Seko Fofana wa Cote d’Ivoire na Al Nassr, Chancel Mbemba wa DR Congo na Olympique Marseille, Fiston Mayele wa DR Congo na Pyramids, Serhou Guirassy wa Guinea na VfB Stuttgart, Yves Bissouma Mali na Tottenham Hotspur, Peter Shalulile wa Namibia na Mamelodi Sundowns,

Mchezaji wa Tunisia Mohamed Ali Ben Romdhane anayechezea klabu ya Ferencvaros ndiye nyota pekee wa Tunisia kwenye orodha hiyo.

Tuzo hizo za kifahari za zinazolenga kuwatuza na kuwasherehekea wachezaji, viongozi na wasimamizi wa kipekee zitaandaliwa tarehe 11 Desemba 2023 mjini Marrakech, nchini Morocco.

TRT Afrika