Mshambuliaji wa Nigeria Victor Osimhen amerejea Napoli kutoka Afcon kwa mpigo na kujitambulisha kwa kuisawazishia Napoli kupitia bao lake lililowapa mabingwa wa ligi ya Italia sare ya 1-1 dhidi ya Barcelona mechi ya hatua ya 16 ya mwisho, Ligi ya Mabingwa.
Osimhen alifunga goli hilo zikiwa zimesalia dakika 15 mechi ya mkondo wa kwanza uliofanyika uwanja wa Stadio Diego Armando Maradona ikiwa mechi yake ya kwanza tangu arudi kutoka Kombe la Mataifa ya Afrika.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alisawazisha bao la Robert Lewandowski la dakika ya 60, na shuti ya kwanza na pekee ya Napoli kwenye goli ambalo lilionekana kuamua matokeo kwani Barca walikuwa ndio timu bora mechini kwa muda mrefu.
Kabla ya kwenda Afcon, Osimhen aliichezea Napoli mara ya mwisho katika ushindi wa 2-0 wa Roma dhidi ya Napoli kabla tu ya Krismasi, wakati alikuwa mmoja wa wachezaji wawili kutoka timu yake waliolishwa kadi nyekundu.
Goli lake la tisa la klabu hiyo msimu huu lilikuja kipindi muhimu, sio tu kwenye mechi lakini katika kampeni ya Napoli wanaocheza chini ya kocha wao wa tatu ndani ya msimu, Francesco Calzona.
Calzona alikuwa na chini ya masaa 48 kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza akiwa zamuni baada ya kuchukua nafasi ya Walter Mazzarri Jumatatu usiku.