Na Suleiman Jongo
TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania
Mashabiki wa klabu ya Yanga nchini Tanzania wamefurahia sana kufuzu kwa timu hiyo katika hatua ya makundi ikiwa ni baada ya miaka 25 tangu timu hiyo ifuzu mara ya mwisho mwaka 1998.
Leo wapinzani wa Yanga Simba wanapambana na Power Dynamo ya Zambia katika kugombania kufuzu hatua hiyo hiyo ya makundi ya kombe la Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Ushindi wa Jumamosi dhidi ya Al-Merreikh ya Sudan wa magoli ya jumla 3-0 uliwaacha wengi hoi kwa furaha isiyo na kifani.
“Tuna furaha sana kuona timu yetu inaendelea kufanya vizuri katika ligi na michuano ya kimataifa,” amesema shabiki mmoja.
“Furaha ya leo haina mfano na kila msemaji wetu akisema ni kweli inatokea.Alituahidi ushindi na kweli tumeupata,”amesema Ally Malik, shabiki kindakindaki wa Yanga.
Shabiki mwingine Samwel Godfrey amesema kinachobaki ni Yanga kujipanga vizuri ili kuhakikisha klabu inasonga mbele.
“Tunamuomba kocha ( Miguel Gamondi) azidi kukinoa vizuri kikosi maana sasa tunakwenda katika hatua ngumu ya ushindani,” alisema Godfrey. ''Tayari Yanga imejenga hofu kwa wapinzani,lakini inabidi tufanye kweli tunapokutana nao,”ameongeza.
Ushindi wa Yanga wa goli 1-0 wa nyumbani kupitia goli lililofungwa na Clement Mzize uliowapa matokeo ya jumla ya 3-0 baada ya matokeo ya awali ya Rwanda na kuwapa furaha mamilioni ya mashabiki wa timu hiyo, ambayo mara ya mwisho ilifuzu hatua hiyo mwaka 1998.
Akizungumza mara baada ya mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Chamazi, Naibu Waziri wa Michezo Hamisi Mwinjuma amesema Yanga imefanya kile ambacho Serikali inatarajia.
“Tunaweka mkazo katika kila mchezo na tumeona namna diplomasia ya michezo inavyolainisha siasa,” alisema Waziri Hamisi. “Watu wanakuwa na amani, furaha na upendo na kuweka kando itikadi zao,”
“Siku zote, kama Serikali, tutaendelea kuunga mkono jitihada za uwekezaji wa vilabu ili viendelee kufanya vizuri katika michezo,” aliongezea Mwinjuma.
Ushindi huu umeifanya Yanga kutangulia hatua ya Makundi na wanajiunga na timu nyingine za TP Mazembe ya Jamhuri ya watu wa Kongo ( DRC), Mamelodi Sundown ya Afrika ya Kusini, Jwaneg Galaxy ya Botswana, na timu mbili za Al Ahly na Pyramids za Misri.
Timu hizi kila moja imejihakikishia kiasi cha dola 700,000 ( zaidi ya shilingi bilioni 1.8) kwa kufuzu hatua ya makundi.
Kwa upande wa Tanzania, timu zilizobaki katika kinyang’anyiro cha kufuzu ni Simba na Singida Big Stars.
Uwanja uliochezewa mechi wa Chamazi una uwezo wa kuchukua mashabiki takriban 20,000