Shirikisho la soka barani Afrika (CAF), limeiadhibu klabu ya USM Alger kutoka Algeria na kuipa klabu ya Morocco RS Berkane, ushindi wa 3-0.
Aidha, CAF imetangaza kuwa kesi hiyo itawasilishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya CAF.
Kamati ya Mashindano ya Klabu za CAF na Usimamizi wa mfumo wa leseni ya klabu imefikia uamuzi wa kuiadhibu Usm Alger matokeo ya kupoteza 0-3 dhidi ya RS Berkhane.
Hii ni baada ya mzozo juu ya jezi ya timu kusababisha mechi ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF, kati ya USM Alger na RS Berkane kutoka Morocco, iliyopangwa kuchezwa, Algiers, Algeria, kufutwa kabla ya timu hizo kushuka dimbani.
Awali, vyombo vya habari vya Algeria viliripoti kwamba maafisa wa nchi hiyo walizuia jezi za Berkane kwa misingi ya kwamba zilikuwa na ramani ya Morocco ambayo ilijumuisha eneo la Sahara Magharibi lenye utata.
Vilevile, CAF limeongeza kuwa, mchuano wa mkondo wa pili utaendelea kama ulivyopangwa Jumapili ya Aprili 28 katika uwanja wa manispaa wa Berkane nchini Morocco.