Mashujaa wa nchi, Tanzania maarufu “Taifa Stars” wamewasili Dar es salaam kutoka Annaba, Algeria baada ya kufunga kazi kwa kufuzu Afcon 2023 kwa kutoka sare ya 0-0 na wenyeji Algeria katika mchuano wao wa mwisho wa hatua ya makundi .
Miamba hao wa soka walipokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu.
"Tunawashukuru sana Watanzania wote kwa kutupokea vyema na kwa pongezi zao. Tunamshukuru pia Mheshimiwa rais wetu Samia Suluhu kwa kuipa timu motisha kupitia wizara yetu. Katika hatua za kambi, na safari nzima hadi kufuzu Afcon. Kazi haikuwa rahisi, mpaka kufuzu." Saidi alifafanua.
Donge nono la Milioni 500
"Hata kabla ya mechi alikuwa ametimiza ahadi yake ya shilingi milioni 500 ili tuziwasilishe kwa timu, kwa safari hii na kwa kazi nzuri iliyofanyika." Alisema.
Uangalizi wa serikali kwa Taifa Stars utakuwa mkubwa zaidi
"Serikali itakuwa bega kwa bega na TFF ili tufike mbali. Tunavyoenda mbele, ufadhili, jicho na uangalizi wa serikali kwa timu hii chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu na viongozi wa wizara na baraza la michezo utakuwa mkubwa zaidi." Saidi Yakubu alisema.
"Timu yetu imefuzu mara ya tatu, na mpira wetu umekua sana. Tutajitahidi zaidi kutekeleza na kuandaa utaratibu na TFF ili kutimiza mahitaji ya kocha na timu kule Ivory Coast.
Wito kwa watanzania kuendelea kuiunga mkono timu hiyo.
"Tutafanya kazi na TFF ili kuhakikisha mashabiki wetu wametuunga mkono kule Abidjan," Saidi aliongeza.
"Watanzania wengi walijitokeza Cairo 2019, na safari hii tunataka wajitokeza zaidi," katibu Saidi alikariri.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, kiungo wa Taifa Stars John Bocco ametoa shukrani kwa wapenzi wa soka Tanzania na serikali ya nchi hiyo ikiongozwa na Rais Samia Suluhu kwa uungwaji mkono na kuwewezesha hadi kufuzu kwa Afcon.
"Tunamshukuru mwenyezi mungu kwa kutufikisha Afcon na Watanzania wote kwa jumla kwa kusimama na sisi muda huo wote katika michuano ya kufuzu pamoja na Rrais wetu Mama Samia kwa kutuunga mkono na kutupa motisha hadi ufanisi huu wetu," alisema.
Kwa upande wake, mkufunzi wa Tanzania ambaye aliandikisha historia na Taifa stars kwa kuwarudisha Afcon tangu 2019, Adel Amrouche, amewashukuru wadau wote wa michezo na serikali ya Tanzania kwa kuiwezesha timu hiyo kujiunga na miamba wa soka barani, Abidjan.
"Kwanza kabisa Namshukuru Rais Samia kwa kutuunga mkono katika harakati hii, wizara ya spoti, TFF na wachezaji wetu mashujaa uwanjani. Nafurahia sana ufanisi wetu. Kwa kweli nawashukuru wote waliotupongeza. Kufuzu Afcon ilikuwa lengo langu, ndoto yangu, na goli langu kuu. " Amrouche alisema.