Na Mustafa Abdulkadir
Kocha wa muda wa Manchester United, Ruud van Nistelrooy, ameondoka kwenye nafasi hiyo baada ya kuwasili kwa kocha mpya Rúben Amorim kutoka Sporting Lisbon ya Ureno.
Van Nistelrooy aliiongoza timu katika mechi nne, akishinda mechi tatu na kutoka sare moja.Ikumbukwe kwamba Van Nistelrooy aliwahi kuwa mshambuliaji mahiri wa Manchester United, akiifungia timu hiyo mabao 150 katika mechi 219 alizocheza kati ya mwaka 2001 na 2006.
Alikuwa gwiji wa klabu hiyo, akiacha alama isiyosahaulika kwa mashabiki wa United.
Kocha wa Klabu ya Sporting Lisbon, Rúben Amorim ameteuliwa kama kocha mpya wa Klabu ya Machester United.
Kocha huyo mwenye miaka 39 ameishindia Klabu ya Sporting Lisbon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 19 kombe la Primeira Liga, pia aliwahi kuchezea timu ya taifa ya Ureno.
Hapo awali makocha wengi wataalamu walipewa kazi ya kuifufua Klabu ya Manchester United, baada ya kustaafu kwa Sir Alex Ferguson, lakini wengi hawakufanikiwa.
Mashabiki wa United wanasubiri kuona kama Rúben Amorim ataweza kuwatoa ‘’Shetani Wekundu’’ kutoka kwenye masaibu yao.
Haya yanajiri baada ya Manchester United kumtimua kwa aliyekuwa kocha wa Manchester United Eric ten Hag.