Andros Townsend amegeukia tiba asili huku akitafuta kuukarabati mwili wake na amesifia miguu ya kuku, kuwa siri yake. Picha: Getty

Andros Townsend mwenye umri wa Miaka 32 alijiunga na Luton Town ya Ligi kuu nchini Uingereza, baada ya kukaa nje msimu mzima uliopita na mwisho wa 2021-22 kutokana na majeraha akiichezea Everton.

Winga Andros Townsend wa klabu ya Luton Town amegeukia tiba asili huku akitafuta kuukarabati mwili wake na kuepuka kupata majeraha makubwa ya magoti yaliyomfanya awe nje ya soka kwa muda mrefu.

Wakati miguu ya kuku ni mlo maarufu katika sehemu nyingi za ulimwengu, miguu hiyo haionekani kama chakula cha kawaida kwa mchezaji maarufu wa Ligi Kuu.

"Kila usiku mimi hula miguu ya kuku yenye mvuke kama chakula cha jioni, kwa sababu kuna 'collagen' katika miguu ya kuku," Townsend amesema.

Hata hivyo, Townsend anaamini kwamba chakula hicho kinamsaidia kuwa na afya nzuri kuliko wakati mwingine wowote, pamoja na faida nyingine za ziada anazohisi.

"Mimi huwa ninaagiza miguu ya kuku ikiwa katika mafungu makubwa na inakuja ikiwa imehifadhiwa kisha ninaiweka kwenye jokofu kabla ya kula baadaye," alimaliza.

Winga huyo aliyasema hayo akizungumzia jinsi lishe yake ilivyosaidia kubadilisha maisha yake, wakati wa mahojiano na kipindi cha Fozcast, yanayoendeshwa na kipa Ben Foster.

"Ninaiweka katika tanuri la mvuke kwa dakika 20 na kwa hakika ni nzuri ni kama vipapatio vya kuku," Townsend alisimulia.

Mlo huu wa Townsend, mwenye zaidi ya miaka kumi ya uzoefu wa viwango vya juu ya soka ambapo aliwakilisha timu kama vile Tottenham, Newcastle, Crystal Palace na Everton, umewavutia wengi.

"Ni wazi, huli mifupa lakini inafurahisha hadi unakaribia kula kucha," Townsend alisema.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa England mwenye umri wa miaka 32, Andros Townsend, anatarajia kutafuna miguu ya kuku kunaweza kumsaidia kufanikiwa kwenye kuimarisha matokeo yake ya soka.

TRT Afrika na mashirika ya habari