Rais wa Klabu ya soka ya Morocco Wydad AC, Said Naciri, amekamatwa Ijumaa kama sehemu ya uchunguzi wa biashara ya madawa ya kulevya, mmoja wa mawakili wake alisema.
Naciri, mwenye umri wa miaka 54, alikamatwa kwa amri ya jaji huko Casablanca kwa mashtaka kadhaa ikiwa ni pamoja na "kughushi nyaraka rasmi, kumiliki na kusambaza madawa za kulevya, na matumizi ya hundi bandia," wakili huyo aliiambia AFP, akiomba kutotambuliwa.
Taarifa za vyombo vya habari nchini humo Afrika Kaskazini ziliongeza kwa kusema kuwa, jaji huyo alikuwa amemshtaki Naciri, ambaye ni mwanachama wa chama cha PAM, kwa "utapeli wa pesa".
Uchunguzi huo uliwahusisha washtakiwa 25, 21 kati yao wamekamatwa, akiwemo Abdenbi Bioui, mkuu wa halmashauri ya mkoa wa Oujda mashariki na pia mwanachama wa PAM, wakili huyo alisema.
Naciri anatarajiwa kufikishwa mbele ya hakimu wa uchunguzi kwa mahojiano zaidi Januari 25.
Wakili wa Naciri alisema kuwa uchunguzi dhidi ya mteja wake ulifunguliwa baada ya raia wa Mali, aliyehukumiwa nchini Morocco kwa ulanguzi wa madawa ya kulevya, kumshtaki Naciri kwa vitendo vya uhalifu.