#KOI46 : Basketball: Basket World Cup / Picha: AFP

Sudan Kusini imeaza mechi yake ya ufunguzi ya kihistoria katika Kombe la dunia la Mpira wa Kikapu la FIBA 2023 kwa kupoteza 101-96 dhidi ya Puerto Rico katika muda wa nyongeza kwenye mechi ya Kundi B.

Mchuano huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa Sudan Kusini, iliyoshuhudia safari ya kutia motisha kuanzia kujiunga na FIBA mnamo Desemba 2013, kufika Robo fainali ya mashindano ya FIBA AfroBasket licha ya kuwa mara yake ya kwanza mnamo 2021, na kisha kufuzu kuiwakilisha Afrika Kombe la dunia, FIBA.

Puerto Rico, iliwekeza juhudi za pamoja ya timu hata ingawa Tremont Waters aling'aa mchezo mzima kwa kuitesa Sudan Kusini huku akikusanya pointi 19, na kutoa 'asist'10.

Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Sudan Kusini, Royal Ivey amesema kuwa matokeo hayo ni ya kujipa uzoefu wa kujifunza zaidi kwa timu hiyo.

"Vijana wangu walishindana. Walicheza kwa bidii. Walicheza hadi kipenga cha mwisho. Tunapaswa kuboreka kutokana na hili. Huu ni uzoefu wa kujifunza. Huu ni mchezo wetu wa kwanza. Tuko juu, hatuko chini. Lazima tuwe watulivu." alisema kocha wa Sudan Kusini, Royal Ivey.

Ushauri wa Kuany Kuany

"Ilikuwa mechi ngumu na ni mara yetu ya kwanza kucheza hapa. Puerto Rico walifanya juhudi nyingi na kwetu sisi, tumejifunza kutoka kwa mchezo huu. Tunapaswa kushikamana. kwa kile kinachofanya kazi." Mshambuliaji wa Sudan Kusini Kuany Kuany aliongeza.

Kwa sasa Sudan Kusini inajiandaa kufufua matumaini yake kwenye mechi mbili zilizosalia. itachuana na China kwenye mechi yake ya pili tarehe 28 Agosti kabla ya kumaliza mechi ya makundi tarehe 30 Agosti 30 dhidi ya Serbia.

'Bright Stars' ilifuzu kwa kutoka kundi la Afrika kwa kuandikisha rekodi ya ushindi 11-1, na kuzishinda timu nyingi za Afrika, ikiwa ni pamoja na kuichabanga bingwa wa FIBA AfroBasket, Tunisia mara mbili.

Kwa mara ya kwanza, Kombe la dunia, limeandaliwa kwa pamoja na mataifa mbalimbali huku mechi zikiendelea katika nchi za Ufilipino, Japan na Indonesia.

TRT Afrika