Kocha mkuu wa Sudan Kusini Royal Ivey alisema timu yake ilikuwa "mwangaza" baada ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki ya Paris Jumamosi kama timu iliyoshika nafasi ya juu zaidi barani Afrika katika Kombe la Dunia la Mpira wa Kikapu.
Sudan Kusini, ambao wamefuzu mara ya kwanza kabisa kombe la dunia la mchezo huo, walishiriki mechi yao ya kwanza rasmi ya kimataifa miaka sita pekee iliyopita na wako katika nafasi ya 62 duniani, waliilaza Angola 101-78 mjini Manila na kuambulia ushindi wao wa tatu wa mashindano hayo.
Wapinzani wa karibu zaidi Misri, walipoteza 88-86 dhidi ya New Zealand na kuwawezesha Sudan Kusini kufuzu katika nafasi ya pekee iliyotengewa bara Afrika katika mashindano hayo yatakayofanyika mjini Paris.
Nchi hiyo imekumbwa na misukosuko tangu ilipojinyakulia uhuru mwaka 2011 lakini maonyesho ya timu hiyo katika Kombe la Dunia yamevutia hisia za umma, huku umati wa watu ukikusanyika kutazama kwenye skrini kubwa katika mji mkuu Juba.
Wanavuliwa kofia
Ivey aliyejawa na hisia alisema wameleta "umoja, undugu , upendo na urafiki" nchini.
"Timu hii ni mwanga wa kuigwa. Nchi hii imekuwa huru kwa miaka 12 pekee. Kufanya hivi ni jambo la kushangaza. Ninawavulia kofia wachezaji wangu kwa sababu walituamini tangu siku ya kwanza," alisema.
Sudan Kusini imeshinda sifa kwa nidhamu yao na mtazamo chanya ndani na nje ya uwanja katika Kombe la Dunia linalofanyika Ufilipino, Japan na Indonesia.
Waliambulia ushindi wa kihistoria walipoilaza vigogo China katika mchezo wao wa pili, kabla ya kuwashusha Ufilipino katika hatua ya kuainisha.
Timu 12 pekee zitashiriki mashindano ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Olimpiki ya Paris, huku Ufaransa ikifuzu moja kwa moja kama wenyeji.