Na Lynne Wachira
TRT Afrika, Nairobi, Kenya
Kenya ndiyo nchi ya Kiafrika iliyofanikiwa zaidi katika michezo ya Olimpiki ikiwa na medali 113 za Olimpiki na wanariadha wake wanajivunia sana kutokana na kuvaa jezi za taifa: Nnyeusi, Kijani, Nyekundu na Nyeupe.
Huku michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ikikaribia kwa kasi, rais wa kamati ya kitaifa ya Olimpiki na mshindi mara mbili wa medali ya fedha ya Olimpiki Paul Tergat anapanga ujanja wa kuhakikisha utawala wake utachukua jukumu kubwa katika kupanua urithi tajiri wa riadha huku akirusha mbali zaidi wavu wake kujaribu kunasa medali zaidi.
Tergat analenga medali nje ya mashindano ya riadha na ndondi, michezo ya pekee ambayo Kenya mewahi kushinda medali katika Olimpiki.
Paul Tergat ambaye ni bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon anaongoza Kenya kwenye michezo ya Olimpiki, mara ya pili kama msimamizi wake ametaja maandalizi ya mapema kama ujanja wa pekee wa kufanikisha michezo ya Olimpiki ya 2024.
"Kama mwanariadha wa zamani mtazamo wangu wa mashindano, nikiwa msimamizi unachangiwa na uzoefu wangu kama mwanariadha mahiri,'' amesema Paul Tergat. ''Lengo letu katika kamati ya Olimpiki ya Kenya ni kuweka mazingira mazuri ambayo yanawasaidia wanariadha kuinua uwezo wao, tunapaswa kufanya kila kitu ndani ya uwezo wetu.''
''Uwezo wa kuhakikisha hakuna medali tunapoteza, maandalizi ya mapema ni kiwango cha chini kisichoweza kupunguzwa kwa utawala wangu,'' alifichua Tergat, akiwa ziarani Ufaransa kama kutathmini maandalizi ya michezo hiyo.
Rekodi bora zaidi ya medali kwa Kenya
"Kushinda au kushindwa medali huanza tangu wakati wa maandalizi, hatupotezi lengo letu ambalo ni kushinda medali nyingi zaidi za Kenya katika mchezo mmoja wa Olimpiki." Alitangaza Tergat.
Utendaji bora wa Kenya katika michezo ya Olimpiki ulikuwa katika Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka wa 2008 huku nchi hiyo ikiambulia dhahabu 6, fedha 4 na shaba 6 kwa jumla ya medali 16 na kumaliza katika nafasi ya 13 kwenye jedwali la medali za Olimpiki.
Ziara ya uwanja wa michezo ya Olimpiki ya Paris 2024
Kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 iliweka Februari mwakani kuwa kipindi cha mwisho kwa timu zinazotaka kuzuru uwanja wa Olimpiki kama maandalizi yao, kukusanya tikiti zao, kujifunza juu ya itifaki na masharti na kuweza kuuliza masuali yoyote walionayo kabla ya michezo.
Kenya ilichukua fursa hiyo kwa kusajili timu inayoongoza katika michezo ya Paris kama sehemu ya mpango wake wa michezo ya kabla ya Olimpiki.
Ujumbe wa Paris ulitembelea kijiji cha wanariadha ambacho kwa kiasi kikubwa bado ujenzi unaendelea ingawa maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na ukumbi wa michezo, vifaa vya mafunzo na malazi yanaelekea kumalizika.
Kijiji hicho cha riadha kipo katikati mwa mkoa wa Paris wa Saint-Denis, na kimejengwa juu ya hekta 50 za ardhi katikati ya mito miwili na kina uwezo wa kubeba zaidi ya wanariadha 14,000 na maafisa wakuu wa timu, ambapo baada ya mashindano . kijiji kitageuzwa kuwa sehemu ya kudumu ya utumizi wa umma.
"Nimefurahi kuona kuwa kijiji cha wanariadha kiko vizuri na kina vifaa vya mazoezi, ambayo inamaanisha kuwa wakati wa kusafiri kwenda kumbi za mazoezi utaondolewa, nia yetu hapa imekuwa hasa kuhakikisha tunaweza kuamua eneo bora kwa timu ya Kenya kukaa katika kijiji kama hicho.'' amesema Tergat.
''Tunataka kuwashirikisha waandaaji hapa ili kuhakikisha baadhi ya taaluma zetu zinajumuishwa mapema vya kutosha,” aliongeza Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya wa Michezo ya Olimpiki baada ya kuzuru kijiji hicho cha wanariadha.
Kijiji kipya cha wanariadha kitageuzwa kuwa wilaya mpya ya jiji iliyo na shule, vituo vya biashara na nafasi wazi za kijani na familia 6000 zinazotarajiwa kukaa.
Kama vinara wa riadha, wajumbe wa Kenya walichagua Stade de France kuwa kituo chao cha kwanza cha mashindano. Uwanja huo utakuwa mwenyeji wa mashindano ya Raga na Riadha, matukio mawili ambayo yana mvuto mkubwa kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Timu ya Raga ya Wanaume tayari imefuzu kwa Michezo ya Olimpiki na itakuwa ikishiriki kwa mara ya tatu mfululizo kwenye michezo ya Olimpiki huku Kenya ikiwa taifa la Afrika lenye mafanikio zaidi katika michezo ya Olimpiki huku medali zake nyingi zikizoa katika riadha.
Uwanja wa Stade De France ndio mwanzo umemaliza kuandaa Kombe la Dunia la Raga ambapo Afrika Kusini ilitetea taji lao, kazi ya ukarabati tayari imeanza katika uwanja huo mkubwa zaidi nchini Ufaransa huku lami mpya ikiwekwa katika eneo la kukimbilia katika miezi ijayo.
Meneja Mkuu wa Timu ya Kenya Dimmy Kisalu alipendezwa hasa na masuala mahususi ya Stade de France.
“Nilitaka kubainisha umbali kati ya uwanja wa mashindano, uwanja wa mazoezi pamoja na eneo la kupasha joto, mambo haya yote yatahitajika kuwa. kuweka maanani kwa timu ya ufundi kuweza kupanga mtiririko wa mambo,'' alisema Kisalu.
''Nimefurahishwa sana na ukweli kwamba ilituchukua dakika 5 kuendesha gari kutoka kijijini hadi uwanja chini ya hali ya kawaida ya trafiki, wakati huo utapunguzwa sana na njia maalum ya Olimpiki mwaka ujao,'' aliongezea.
"Tayari ninaweza kuhisi ari ya Olimpiki na ninaweza kuuhakikishia ulimwengu kwamba watashuhudia maonyesho ya Wakenya katika uwanja huu." Alihitimisha Kisalu.
Kenya kulenga Tenisi katika Olimpiki
Uwanja wa Roland Garros, maarufu kwa kuandaa michuano ya French Open utakuwa mwenyeji wa Nusu na Fainali ya Ndondi na ziara ya kutembelea uwanja huo inaonekana kuwasha moto kwa wajumbe wa Kenya huku Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa michezo ya Paris, Wanjiru Karani ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Tenisi Kenya akionyesha kujiamini.
"Nina matumaini makubwa kuwa tutakuwa na mchezaji kwenye michezo ya Olimpiki mwaka ujao, kipindi cha kufuzu bado kinaendelea na nafasi yetu ni nzuri sana," amesema Wanjiru.
Nyota wa Tennis wa Kenya Angela Okutoyi ambaye alishinda taji la vijana la Wimbledon ndiye mtarajiwa bora wa Kenya.
Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Auburn amekuwa akishiriki mashindano mbalimbali ya kitaaluma kabla ya michezo ya Afrika inayotarajiwa kufanyika Machi mwakani ambapo atahitaji kushinda ili kufuzu pia. Aliorodheshwa miongoni mwa wachezaji 500 bora Duniani kufikia mwisho wa kipindi cha kufuzu kwa Olimpiki.
Kenya itaweka kambi Kusini mwa Ufaransa.
Katika ari yake ya maandalizi ya mapema, Kenya ilisaini ushirikiano na Miramas city, mojawapo ya miji rasmi ya mafunzo ya michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Timu ya Kenya imepanga kutumia angalau mwezi mmoja kabla ya kambi ya mazoezi ya Olimpiki mwaka ujao ndipo kuelekea Paris kwa michezo hiyo.
"Kujizoesha ni moja ya mambo muhimu sana linapokuja suala la utendaji, kwa hivyo tulichagua jiji la Miramas kwa sababu litakuwa na hali ya kiangazi sawa na Paris na kwa hivyo ni muhimu kwa timu zetu kukaa huko,'' alisema Tergat.
Miramas ipo katika eneo la Bouche Du'Rhone ambalo linajivunia kutoa wanariadha bora wa Ufaransa akiwemo mshindi wa medali ya shaba ya Dunia Christophe Lemaitre, mmoja wa wanariadha wengine watatu wa Ufaransa walioweza kuvunja kizuizi cha sekunde 10 katika mbio za 100m.