Shirikisho la Mpira wa vikapu la Serbia limetangaza kuwa mshambuliaji wake Simanić alihitajika kufanyiwa upasuaji wa pili wa kuondolewa kwa figo yake iliyojeruhiwa vibaya.
Mshambuliaji Boriša Simanić alipoteza figo kwa sababu ya jeraha alilolipata wakati wa mechi yao siku ya Jumatano dhidi ya Sudan Kusini kwenye Kombe la Dunia la FIBA linaloendelea.
Simanic alipigwa kwenye figo wakati kiungo wa Sudan Kusini Nuni Omot alipokuwa akirusha shuti kupitia mkono wake wa kushoto ili kujitengenezea nafasi na kulenga wavu.
"Samahani, sikukusudia kufanya aina yoyote ya mchezo mchafu. Natumai atapata afueni ya haraka. Ninakuombea, utakuwa katika maombi yangu, " Omot alisema.
"Mimi si mchezaji mchafu, sijawahi kuwa mchezaji mchafu," Omot aliendelea. "Kutoka moyoni mwangu, ninaomba msamaha kwa kila mtu ambaye ananitazama na kwa mchezaji haswa." Omot aliendelea
Aidha, shirikisho la Mpira wa Kikapu, Sudan Kusini pia limetoa taarifa kumuombea afueni huku likisema tukio hilo halikukusudiwa na kutoa maombi na salamu za heri kwa Borisa Simanic.
Kufuatia ajali hiyo, Shirikisho la mpira wa kikapu la Sudan Kusini limesema kuwa mchezaji Nuni Omot amelengwa kwa ubaguzi wa rangi na unyanyasaji kufuatia kusambaa kwa habari juu ya hali ya kusikitisha ya ajali ya figo kwa mchezaji wa Serbia.
"Tunalaani aina yoyote ya ubaguzi wa rangi unaoelekezwa kwa mchezaji Nuni Omot. Mpira wa kikapu ni mchezo unaotambulika kuwaleta watu pamoja badala ya kutumiwa kama zana ya ubaguzi." Shirikisho la Basketboli la Sudan Kusini lilisema.
Safari ya Sudan Kusini katika mashindano
Sudan Kusini, taifa jipya zaidi duniani (lililopata uhuru mwaka 2011), liliingiaa kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la Dunia la Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Kikapu nchini Phillipines na limeweka historia, kufuzu kwa mashindano ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Olimpiki ya 2024.
Huku nchi bado inaekumbwa na vita vikali, timu hiyo ilifanya mazoezi na kucheza nchini Kenya ili kupata kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Imeorodheshwa ya 62 duniani, ilipata nafasi ya kushiriki katika mashindano huko Paris mwaka ujao kama taifa bora la Afrika katika Kombe la Dunia la FIBA linaloendelea.
Ni timu iliyo katika nafasi ya chini zaidi kufuzu kwa mashindano ya Olimpiki ya wanaume tangu mwaka 2004, kulingana na FIBA.