Wachezaji wa Harambee Stars kabla ya mechi yao dhidi ya Qatar. Picha: Facebook: Harambee Stars

Kocha wa timu ya soka ya Harambee Stars Engin Firat amewarai mashabiki wa timu hiyo kuthibitisha uzalendo wao wa kweli vikamilifu kwa kufurika Kasarani wakati miamba hao watakapokuwa wenyeji dhidi ya Sudan Kusini.

Mbali na kocha wa timu hiyo, Rais wa Kenya William Ruto naye ametupa ujumbe huku akiwahimiza mashabiki kujitokeza kujaza uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Kasarani ili kuipa motisha timu ya taifa ya Kandanda kwenye mechi yake ya pili ya kirafiki dhidi ya Sudan Kusin alasiri hii.

Aidha, Rais huyo ametuma pongezi zake rasmi kwa timu haswa kwa kuonyesha soka yenye mvuto na kujizolea ushindi wa 1-2 walipokutana na Qatar ugani Al Janoub, jijini Doha, wiki iliyopita.

Joseph Okumu aliipa kenya uongozi kunako dakika ya 20 baada ya krosi safi kutoka Kenneth Muguna. Hata Hivyo, Qatar ilisawazisha katika dakika ya 34 baada ya Hassan Al-Haydos kufunga kupitia penalti.

Hata hivyo, nguvu mpya Amos Nondi aliyeingia dakika ya 70, kuchukua nafasi ya Masoud Juma, alirejesha uongozi wa Kenya dakika ya 91 na bao la ushindi, baada ya nahodha Michael Olunga kumuandalia pasi mzuri na kuipatia Harambee Stars ushindi wa 2-1.

Kikosi kilichoanza dhidi ya Qatar Wiki iliyopita

Kocha Firat anatarajiwa kudumisha kikosi chake cha juma lililopita dhidi ya Qatar watakaposhuka dimbani dhidi ya Sudan Kusini.

Byrne Odhiambo (GK), Johnstone Omurwa, Joseph Okumu, Eric Ouma, Daniel Anyembe, Richard And, Anthony Akumu, Kenneth Muguna, Masud Juma, Elvis Rupia, Michael Olunga.

TRT Afrika