Nigeria na Equatorial Guinea zilitoka sare ya 1-1 katika mechi yao ya ufunguzi ya hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya 2023 nchini Côte d'Ivoire Jumapili.
Timu hizo mbili ambazo zina pointi moja kila moja, sasa ziko nafasi ya pili katika Kundi A.
Equatorial Guinea walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 36 kupitia kwa mshambuliaji Ivan Salvador.
Nyota wa Napoli, Victor Osimhen aliisawazishia Nigeria dakika mbili baadaye.
Nigeria itamenyana na Côte d'Ivoire mechi yao ijayo
Matokeo yalisalia 1-1 katika muda wote wa mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara.
Wenyeji Côte d'Ivoire, ambao waliilaza Guinea-Bissau 2-0 Jumamosi, wanaongoza Kundi A wakiwa na pointi tatu, huku Guinea-Bissau wakiwa mkiani mwa kundi hilo wakiwa na pointi sifuri.
Nigeria itacheza dhidi ya wenyeji Côte d'Ivoire siku ya Alhamisi, huku Equitorial Guinea ikimenyana na Guinea-Bissau tarehe hiyo hiyo.
Nigeria itacheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Guinea-Bissau Jumatatu, Januari 22, huku Côte d'Ivoire itamenyana na Equatorial Guinea siku hiyo pia.