Mwanasoka wa Australia mwenye asili ya Burundi Nestory Irankunda ameanza mazoezi rasmi na klabu yake mpya ya mabingwa wa ujerumani, Bayern Munich.
Baada ya kuwa na fomu nzuri ya kuvutia katika klabu ya Adelaide United ya Ligi kuu ya soka nchini Australia "A-League" kwa kufunga mabao kadhaa ya kushangaza, Irankunda alianza kusakwa na vilabu mbalimbali akiwa na umri wa miaka 17 tu.
Ingawa alisaini mkataba wake na FC Bayern kwa mkataba wa muda mrefu mnamo Novemba 2023, akiwa na umri wa miaka 17, hangeweza kujiunga nao hadi tarehe 1 Julai 2024 kwani Irankunda alitimiza miaka 18 mnamo tarehe 9 Februari 2024.
Irankunda ameeleza hatua hiyo kuwa ni yenye furaha kubwa kwa familia yake kwani ametimiza ndoto ya baba yake, ambaye amekuwa akimsukuma kucheza soka ya kulipwa barani ulaya.
Mshambuliaji huyo aliyezaliwa Tanzania 2006, alikaribishwa vyema na wenzake wa Bayern huku wakijiandaa kwa msimu ujao chini ya mkufunzi mpya Vincent Kompany.
Irankunda amewashukuru wachezaji wa Bayern kwa kumpokea vyema,"Walinikaribisha sana na kunirahisishia kuwajua.”
Kujifunza Kijerumani
"Nimeanza kujifunza kijerumani muda mfupi baada ya kufika huku kwani, ingawa awali nilijifunza shuleni, nimesahau kwa kiwango kikubwa.”
Irankunda ambaye ni mtoto wa nne kati ya saba, alizaliwa katika kambi ya wakimbizi Kigoma nchini Tanzania, kabla ya wazazi wake Gideon na Dafroza kuhamia Australia alipokuwa na umri wa miezi mitatu tu na kupewa hifadhi nchini humo.
Hata hivyo, ndoto za Burundi kupata huduma za nyota huyo zimedidimia kwani Nestory Irankunda ameiwakilisha timu ya taifa ya soka ya Australia kwa mechi yake ya kwanza ya timu ya taifa, akiingia uwanjani dhidi ya Bangladesh, kabla ya kufunga goli lake la kwanza kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Palestina mnamo Juni 2024.