Wan Bissaka DRC

Beki wa Manchester United Aaron Wan-Bissaka amefuatwa na shirikisho la soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DR Congo, huku akiwaza kubadili uwakilishi wake wa kimataifa kuichezea DRC.

Aaron Wan Bissaka anafuzu kuiwakilisha DRC kwani hajawahi kuiwakilisha Uiengereza kwenye kikosi chake kikuu.

Aidha, mnamo 2015 aliiwakilisha DRC katika ngazi ya wachezaji chipukizi lakini baadae alibadili uwakilishi na kuichagua nchi yake ya kuzaliwa, Uingereza na hata kuiwakilisha kwenye ngazi ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21.

Kwa mujibu wa jarida la Uiengereza la The Athletic, DR Congo wamekuwa wakimshawishi Wan-Bissaka ili kuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Congo kitakachoshiriki Kombe la AFCON 2024.

Wan-Bissaka huenda akajumuishwa kikosi cha kocha wa DRC Sébastien Desabre na kupiga jeki kikosi hicho kinacholenga kufanya vyema kwenye Dimba la Afcon litakaloanza Januari.

Aidha, baada ya kutopewa nafasi kikosi cha the three lions, Wan-Bissaka anasemekana kuwaza kutimiza ndoto za DRC kutokana na ushindani mkali na foleni kwenye nafasi ya beki wa kulia yenye Kyle Walker, Kieran Trippier, Trent Alexander-Arnold, Reece James na Tino Livramento.

Wachezaji wengine wa kimataifa walioichagua DRC ni Arthur Masuaku, Cedric Bakambu na Yannick Bolasie, ambaye aliisaidia Leopards ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kumaliza katika nafasi ya tatu katika Kombe la mataifa bora Afrika 2015.

Hata hivyo, wachezaji wengine walio na asili ya DRC lakini wakawakilisha mataifa mengine ni pamoja na Romelu Lukaku Bolingoli, Vincent Kompany, Steve Mandanda, Youri Tielemans, Michy Batshuayi, Christian Benteke, Presnel Kimbembe.

DRC ilikaribia kucheza Kombe la Dunia 2022, kabla ya kuondolewa na Morocco katika mechi za raundi ya mwisho kufuzu Kombe la Dunia 2022 baada ya kupoteza 4-1 katika mechi ya mkondo wa pili wa mchujo licha ya kutoka sare 1-1 Kinshasa.

Timu ya DRC imekuwa na fomu nzuri chini ya Sébastien ambapo Congo imeanza safari ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwa kuilaza Mauritania 2-0 mnamo Novemba 15, ugani Martyrs, Kinshasa (DR Congo).

DR Congo inatafuta kufuzu Kombe la dunia kwa mara ya pili tangu iliposhiriki Kombe hilo hapo zamani, Ujerumani Magharibi mnamo 1974.

TRT Afrika