Morocco inaingia kombe la Mataifa ya Afrika litakaloanza mwezi ujao, Cote D'ivoire 2023, ikiwa timu iliyoorodheshwa zaidi katika mashindano hayo kufuatia kutolewa kwa viwango vya FIFA Alhamisi iliyopita.
Wiki chache tu baada ya Simba wa Atlas kutawazwa kuwa kikosi bora cha mwaka wa kandanda katika kipindi kati ya Novemba 2022 hadi Septemba 2023 na Shirikisho la Soka barani CAF, Morocco inafunga mwaka kuwa timu bora kulingana na orodha ya viwango kutoka FIFA.
Morocco ilipewa tuzo ya Timu bora ya Taifa ya mwaka kwa mara yao ya kwanza kipindi ambacho taifa hilo limejivunia ufanisi usiomithilika ndani na nje ya bara la Afrika.
Mnamo mwezi Novemba, timu ya taifa ya soka ya Morocco ilishinda tuzo ya timu bora ya Afrika kutoka Muungano wa Mashirikisho ya Michezo Afrika (AUCSA) mjini Cairo.
Taifa hilo lilipongezwa pakubwa baada ya timu ya taifa ya wanaume kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia FIFA Qatar 2022.
Morocco pia imekabidhiwa zabuni ya kuandaa Kombe la Dunia FIFA 2030 ikishirikiana na Uhispania na Ureno.
Timu ya Morocco U-23 ilitunukiwa ubingwa wa kombe la mataifa ya Afrika na hata kujikatia tiketi ya Michezo ya Olimpiki Paris 2024 ya mwaka ujao.
Katika mataifa 10 bora barani kwa mujibu wa viwango vya FIFA, Morocco inafuatwa na Senegal, Tunisia, Algeria, Misri, Nigeria, Cameroon, Cote D'ivoire, Mali na Burkina Faso ambao wanakamilisha nchi kumi bora.